NIGERIA-USALAMA

Nigeria: Wanajihadi washambulia kambi ya UN kaskazini mashariki

Kwa zaidi ya muongo mmoja jeshi la Nigeria linaendelea kukabiliana wanamgambo wa Kiislamu, vita ambavyo vimeathiri eneo la Kaskazini Mashariki, na kuua watu wasiopungua 36,000 na wengine zaidi ya milioni mbili kuyahama makazi yao.
Kwa zaidi ya muongo mmoja jeshi la Nigeria linaendelea kukabiliana wanamgambo wa Kiislamu, vita ambavyo vimeathiri eneo la Kaskazini Mashariki, na kuua watu wasiopungua 36,000 na wengine zaidi ya milioni mbili kuyahama makazi yao. STEFAN HEUNIS AFP/File

Wapiganaji wa kundi la ISWAP, tawi la Boko Haram yenye mafungamano na kundi la Islamic State, walivamia mji wa Dikwa, unaopatikana kilomita 100 kutoka Maiduguri, mji mkuu wa jimbo la Borno - na kushambulia kambi ya jeshi na kituo cha misaada cha Umoja wa Mataifa ambapo wafanyakazi 25 wa wa mashirika ya kutoa msaada wamekimbilia, kulingana na vyanzo vya usalama.

Matangazo ya kibiashara

Shambulio la jana usiku lilikuwa lilitekelezwa kwa haraka na lilikuwa la kushangaza, amebaini mwandishi wetu huko Lagos, Liza Fabbian: Wanajihadi wa kundi la ISWAP walivamia mji wa Dikwa na kuanza kuzishambulia kambi mbili ile ya jeshi la Nigeria na kambi ya kikosi cha wanajeshi wa Umoja wa Mataifa.

"Magaidi wa ISWAP walizindua mashambulizi mawili kwa wakati mmoja kwenye kambi kubwa jeshi na kituo cha misaada cha Umoja wa Mataifa," kulingana na chanzo cha jeshi kilichonukuliwa na shirika la habari la AFP.

Jeshi liliingilia kati kujaribu kuwatimua washambuliaji, kwa msaada wa ndege na helikopta. Wanajeshi wengi pia walipelekwa kutoka mji wa karibu wa Marte - ambao ulichukuliwa wiki iliyopita na jeshi la Nigeria kutoka mikononi mwa kundi ISWAP walioudhibiti wiki moja iliyopita.

"Kituo cha misaada cha Umoja wa Mataifa kimeteketezwa kwa moto na wapiganaji lakini hadi sasa hakuna mfanyakazi yeyote aliyeuawa au kujeruhiwa," chanzo cha kutoka mashirika ya misaada kimeliambia shirika la habari la AFP. "Tuna wafanyakazi 25 ambao wamekimbilia kwenye jumba la kulala, ambalo waasi wanajaribu kuvamia sasa," chanzo hiki kimesema, kikithibitisha habari kutoka kwa afisa wa jeshi.

Miaka mitatu iliyopita, mnamo Machi 1, 2018, wapiganaji wa ISWAP walishambulia kituo cha Umoja wa Mataifa katika mji wa Rann, Kaskazini Mashariki mwa Nigeria. Maafisa wanane wa vikosi vya usalama waliuawa pamoja na wafanyakazi watatu wa UNICEF, raia ​​wa Nigeria na Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM).

Shambulio hili jipya usiku wa jana katika mji wa Dikwa bado ni ishara nyingine ya kuzorota vibaya kwa hali ya usalama kaskazini mashariki mwa Nigeria.