SENEGAL-SIASA-HAKI

Senegal yazima intaneti, maandamano yaongezeka

Mbele ya kituo cha redio cha RFM baada ya kupita kwa waandamanaji. Dakar, Machi 5, 2021.
Mbele ya kituo cha redio cha RFM baada ya kupita kwa waandamanaji. Dakar, Machi 5, 2021. AFP - JOHN WESSELS

Mamlaka nchini Senegal imetoa agizo kwa mashirika yanayotoa huduma ya mtandao kuzima intaneti nchi nzima, wakati maandamano dhidi ya kuzuiliwa kwa kiongozi wa upinzani yanazidi kuongezeka, shirika la kuangalia mtandao NetBlocks limeripoti leo Ijumaa.

Matangazo ya kibiashara

Kulingana na NetBlocks, huduma ya intaneti kwa mitandao ya kijamii na programu za ujumbe, ikiwa ni pamoja na Facebook, WhatsApp na YouTube, imezimwa mapema Ijumaa, kabla ya maandamano yaliyoandaliwa kwa mwito wa wawakilishi wa vyama vya kiraia na chama.upinzani vinavyjumuika katika vuguvugu la "Y'en a marre".

Katika siku mbili zilizopita, angalau mtu mmoja aliuawa katika makabiliano kati ya polisi na wafuasi wa mwanasiasa wa upinzani Ousmane Sonko, ambaye anakabiliwa na mashtaka ya ubakaji na ambaye kukamatwa kwake kulichochewa kisiasa, kulingana na wafuasi wa mwanasiasa huyo.

"Tunatoa wito kwa mamlaka nchini Senegal kuheshimu uhuru wa mkusanyiko wa amani kote nchini," amesema mkurugenzi wa shirika la kimataifa  la haki za binadamu la Amnesty Internationa katika ukanda huo, Samira Daoud.

Ousmane Sonko, 46, mkaguzi wa zamani wa ushuru, ambaye alichukuwa nafasi ya tatu katika uchaguzi wa urais wa mwaka 2019 kwa 15% ya kura, anaungwa mkono na vijana wa Senegal.

Mpinzani huyo alikamatwa Jumatano kwa kosa la "kuhatarisha usalama wa nchi" kufuatia maandamano ya kumuunga mkono kote nchini.

Mwezi uliopita mfanyakazi wa saluni alimshtaki kuwa alimbaka. Aliitishwa kufika kuripoti mahakama baada ya kinga yake ya bunge kuondolewa wiki iliyopita.

Ousmane Sonko aliishutumu serikali ya rais Macky Sall kwa kuhusika na malalamiko ya ubakaji ili kumuangusha kisiasa.