ETHIOPIA-TIGRAY

Mwanadiplomasia wa Ethiopia nchini Marekani ajiuzulu

Waziri mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed
Waziri mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed REUTERS/Kumera Gemechu

Mwanadiplomasia wa Ethiopia anayehudumu katika Ubalozi wa nchi hiyo nchini Marekani, ametangaza kujiuzulu kufuatia mzozo unaoendelea katika jimbo la Tigray.

Matangazo ya kibiashara

Kupitia barua yake, Mwanadiplomasia huyo Berhane Kidanemariam, amesema hawezi kuendelea kuhudumu katika nafasi hiyo, kwa kile alichokitaja ni kuendelea kwa vita vya halaiki katika jimbo la Tigray.

Najiuzulu kwenye nafasi yangu, kuonesha gadhabu kuhusu vita vya halaiki huko Tigray, na kupinga pia mateso na uharibifu unaofanywa na serikali katika maeneo mengine ya Ethiopia.

Aidha, kwenye barua yake amesema miundo mbinu katika jimbo hilo, imeharibiwa sana, na kuwashtumu wanajeshi wa serikali kwa kuwabaka wanawake na wasichana na kusababisha vifo vya maelfu ya watu, wengine wakisalia wakimbizi.

Serikali ya Ethiopia na Eritrea, zimeendelea kukanusha madai ya vikosi vyao kuhusika na uhalifu wa kivita katika jimbo hilo, wakati huu mashirika ya kimataifa ya kutetea haki za binadamu, ikiwemo Marekani, yakitaka uchunguzi huru kufanyika katika jimbo hilo.

Waziri Mkuu Abiy Ahmed alituma jeshi  la nchi hiyo kwenda kupamnana na vikosi vya Tigray People's Liberation Front (TPLF), kwa kile alichosema kuwa vilishambulia kambi za jeshi nchini hmo.