ETHIOPIA

Abiy Ahmed: Ni kweli wanajeshi wa Eritrea wako Tigray

Abiy Ahmed alitangaza ushindi mnamo Novemba 28, lakini baadhi ya viongozi wa TPLF wako mafichoni na wameapa kuendelea na mapigano.
Abiy Ahmed alitangaza ushindi mnamo Novemba 28, lakini baadhi ya viongozi wa TPLF wako mafichoni na wameapa kuendelea na mapigano. Amanuel Sileshi AFP

Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed amekiri kuwapo kwa wanajeshi wa Eritrea katika jimbo la Tigray, na aamesema "haikubaliki" mashambulio yanayowezekana kwa raia ambayo wanaweza kuwa yamefanya katika eneo hili la mpaka linalokumbwa na mapigano tangu mwezi Novemba 2020.

Matangazo ya kibiashara

Uwepo wa wanajeshi kutoka Eritrea  katika jimbo la Tigray uliripotiwa na wakaazi, mashirika yasiyo ya kiserikali na wanadiplomasia kadhaa, lakini madai hayo yalikanushwa kwa miezi kadhaa na mamlaka ya nchi zote mbili.

"Baada ya jeshi la Eritrea kuvuka mpaka na kuendesha operesheni za kijeshi nchini Ethiopia, uharibifu wowote uliohujumu raia wetu haukubaliki," Abiy ameliambia bunge Jumanne wiki hii.

"Hatukubali kitendo hicho kwa sababu ni jeshi la Eritrea, na hatungekubali kama ingelikuwa ni askari wetu. Operesheni ya kijeshi ilikuwa dhidi ya maadui wetu waliolengwa wazi, sio dhidi ya raia. Tuliijadili hilo mara nne au mara tano na Serikali ya Eritrea, ”ameongeza.

Raia wa Tigray yashtumu vikosi vya Eritrea

Wakazi wa Tigray wameripoti kwa mashirika ya haki za binadamu na waandishi wa habari juu ya mauaji na unyanyasaji wa kijinsia unaofanywa dhidi ya raia na vikosi vya usalama, pamoja na wanajeshi wa Eritrea.

Bwana Abiy, mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel mnamo mwaka 2019, mapema mwezi Novemba alizindua operesheni ya kijeshi iliolenga kupindua chama tawala katika mkoa huu wa kaskazini mwa nchi, Tigray People's Liberation Front (TPLF), ambachoo alikishutumu kuwa vikosi vyake vilitekeleza shambulio dhidi ya kambi za jeshi.

Alitangaza ushindi mnamo Novemba 28, lakini baadhi ya viongozi wa TPLF wako mafichoni na wameapa kuendelea na mapigano.

Eritrea yaingia vitani kutokana na TPLF

Kulingana na kiongozi wa serikali ya Ethiopia, mamlaka nchini Eritrea inasema TPLF iliwashinikiza kuingia katika vita hivyo "kwa kurusha roketi" nchini mwao kutoka eneo la mpakani.

"Eritrea ilituambia kuwa ina changamoto za kiusalama wa kitaifa na kwa hivyo iliteka maeneo ya mpaka," Abiy amesema.

Ameelezea kuwa serikali ya Eritrea inadai wanajeshi wake waliteka mifereji ya eneo la mpakani iliyochimbwa wakati wa vita vilivyotokana na tatizo la mpaka katika miaka ya 1998-2000 kati ya mataifa hayo mawili, ambalo lilikuwa limeachwa na wanajeshi wa Ethiopia.

Kulingana na Bwana Abiy, mamlaka ya Eritrea imeahidi kuondoka ikiwa wanajeshi wa Ethiopia watarudi kwenye nchini mwao.

"Serikali ya Eritrea imelaani vikali madai hayo ya unyanyasaji na kusema itachukua hatua dhidi ya askari yeyote inayotuhumiwa," ameongeza.