MSUMBIJI

Mashambulizi nchini Msumbiji: Palma mikononi mwa wanajihadi

Watu wengi wameyatoroka makaazi yao katika vijiji mbalimbali na kukimbili katika mji wa Cabo Delgado, Msumbiji
Watu wengi wameyatoroka makaazi yao katika vijiji mbalimbali na kukimbili katika mji wa Cabo Delgado, Msumbiji Alfredo Zuniga AFP

Mji wa Palma, ulioko kaskazini mashariki mwa Msumbiji, kilomita kumi tu kutoka eneo kunakoendeshwa mradi mkuu wa gesi unaosimamiwa na kampuni ya mafuta ya Ufaransa TOTAL, sasa uko mikononi mwa wanajihadi baada ya siku tatu za mapigano, vyanzo vya usalama vimebaini.

Matangazo ya kibiashara

"Vikosi vya serikali vimejiondoa katika mji wa Palma, kwa hivyo mji huo unadhibitiwa" na makundi yenye silaha ya kijihadi tangu jana usiku, moja ya vyanzo hivi vimeliambia shirika la habari la AFP.

"Mji wa Palma unashikiliwa na washambuliaji," kiliongeza chanzo kingine ambacho kimetaka jina lake lisitajwe, kikisema mapigano yanaendelea katika eneo hilo.

Jimbo lenye Waislamu wengi la Cabo Delgago, ambalo ni tajiri kwa gesi asilia, limekuwa likikabiliwa na vita vikali vya msituni kwa zaidi ya miaka mitatu. Mji wa Palma, ambapo maelfu ya watu wamekimbilia baada ya kutoroka vijiji vyao kutokana na vurugu, kwa sasa lina wakaazi 75,000.

Siku ya Jumatano alasiri, makundi haya yenye silaha ya kijihadi, ambayo yalikuwa yakijificha katika miezi ya hivi karibuni, yalianzisha shambulio kubwa katika mji huo, siku ambayo kampuni ya mafuta ya TOTAL ilitangaza kuanza tena shughuli zake kwenye eneo inalokuwa tarajia kuchimba gesi mnamo mwaka 2024.

Watu kadhaa wameuawa, kulingana shirika la kimataifa la haki  la Human Rights Watch, likinukuu mashahidi "ambao wamesema wameona miili barabarani". Raia mmoja wa Afrika Kusini ni miongoni mwa watu hao waliouawa, kulingana na chanzo cha serikali huko Johannesburg.