NIGER

Niger: "Hali yadhibitiwa" baada ya milio ya risasi karibu na makaazi ya rais

Washambuliaji kutoka kambi ya kikosi cha anga cha 101 mjini Niamey wakiwa katika magari matatu walishambulia kituo cha kwanza cha kikosi cha walinzi wa rais, ambacho kilijibu kwa bunduki za kivita na makombora.
Washambuliaji kutoka kambi ya kikosi cha anga cha 101 mjini Niamey wakiwa katika magari matatu walishambulia kituo cha kwanza cha kikosi cha walinzi wa rais, ambacho kilijibu kwa bunduki za kivita na makombora. © Wikimedia Commons CC BY 2.0 Jean Rebiffé

Milio ya risasi imesikika usiku wa Jumanne Machi 30 kuamkia leo Jumatano, karibu na makaazi ya rais mjini Niamey, nchini Niger. Kulingana na vyanzo vya usalama, lilikuwa "jaribio la mapinduzi" ambalo lilitibuliwa haraka na kikosi cha walinzi wa rais siku mbili kabla ya kuapishwa kwa rais Mteule Mohamed Bazoum.

Matangazo ya kibiashara

Wakaazi wa mji mkuu wa Niger, Niamey wamesema wamesikia milio ya risasi katika maeneo yanayoizunguka Ikulu ya rais usiku wa kuamkia leo Jumatano 31.03.2021.

Kulingana na wakaazi hao, milio hiyo ya silaha ilisikika katika wilaya ya Plateau yalipo makaazi rasmi ya rais pamoja na ofisi yake.

Washambuliaji kutoka kambi ya kikosi cha anga cha 101 mjini Niamey wakiwa katika magari matatu walishambulia kituo cha kwanza cha kikosi cha walinzi wa rais, ambacho kilijibu kwa bunduki za kivita na makombora. Urishianaji risasi ulidumu dakika kumi na tano hadi ishirini, kulingana na mashahidi.

Washambuliaji kadhaa walikamatwa. Hivi sasa wanahojiwa katika makaomakuu ya polisi.

Mohamed Bazoum alitangazwa mshindi rasmi wa duru ya pili ya uchaguzi wa urais wa Februari 21. Ushindi wake bado haujatambuliwa na mpinzani wake wa kisiasa Mahamane Ousmane.