CHAD

Chad yajiandaa kwa uchaguzi wa Jumapili

Uchaguzi wa urais Chad umepangwa kufanyika April 11.
Uchaguzi wa urais Chad umepangwa kufanyika April 11. © AFP - Gael COGNE

Tume ya uchaguzi nchini Chad inasema kuwa maandalizi yote yamekamilika, kuelekea uchaguzi wa urais utakaofanyika siku ya Jumapili Aprili 11.

Matangazo ya kibiashara

Rais wa muda mrefu Idriss Derby Itno ambaye amekuwa madarakani kwa zaidi ya miaka 30, anatarajiwa kurejea tena madarakani.

Rais anayemaliza muda wake Idriss Déby Itno wakati wa kampeni yake ya uchaguzi huko Ndjamena, Machi 13, 2021.
Rais anayemaliza muda wake Idriss Déby Itno wakati wa kampeni yake ya uchaguzi huko Ndjamena, Machi 13, 2021. AFP - RENAUD MASBEYE BOYBEYE

Hivi karibuni kiongozi wa chama cha upinzani cha Transformateurs nchini Chad alitoa wito wa kususiwa uchaguzi mkuu ujao wa Aprili 11 akiutaja kuwa ni wa kimaonyesho tu.

Dkt Succès Masra ambaye alikuwa akihutubia waandishi wa habari katika makao makuu ya chama hicho mjini N'Djamena aliituhumu serikali ya rais Idriss Deby kuwa inanyanyasa wapinzani na kuwaonyesha waandishi habari mabaki ya risasi ambazo amesema zilifyatuliwa na polisi kwenye mkutano wa kisiasa wa vyama vya upinzani.

Masra amesema zoezi lililopangwa kufanyika tarehe 11 ni utani na mchezo na kwa msingi huo kambi ya upinzani inafanya kila liwezekanalo kuhakikisha kwamba uchaguzi huo unasusiwa na wananchi.

Mkutano kati ya rais wa Chad Idriss Déby na mpinzani wake Succès Masra, Machi 16, haukupokelewa vyema na wafuasi wa mwanasiasa huyo wa upinzani.
Mkutano kati ya rais wa Chad Idriss Déby na mpinzani wake Succès Masra, Machi 16, haukupokelewa vyema na wafuasi wa mwanasiasa huyo wa upinzani. © capture d'écran Twitter