Mohamed Farmajo kuendelea madarakani kwa miaka miwili

Rais wa Somalia Mohamed Abdullahi Mohamed, maarufu kama  Farmajo
Rais wa Somalia Mohamed Abdullahi Mohamed, maarufu kama Farmajo Riccardo Savi / GETTY IMAGES NORTH AMERICA / AFP

Wabunge nchini Somalia, wamepitisha mswada wa kumwongezea muda wa kuongoza rais Mohamed Farmajo kuendelea kuwa madarakani kwa miaka miwili.

Matangazo ya kibiashara

Mswada huo sasa sasa unasubiri uungwaji mkono wa bunge la Senate, na tayari uongozi wa bunge hilo umesema mswada huo ni kinyume cha sheria, hatua ambayo imeungwa mkono na baadhi ya Maseneta.

Hatua ya wabunge nchini Somalia, imekuja baada ya serikali ya rais Farmajo kushindwa kuandaa uchaguzi mwezi Februari mwaka huu baada ya muda wake kumalizika.

Juhudi za kuwepo kwa maelewano kati ya wanasiasa nchini humo hasa kati ya uongozi wa Mogadishu na wakuu wa serikali ya serikali ya majimbo chini ya wawakilishi wa Umoja wa Mataifa, kutafuta mwafaka wa namna ya kufanikisha uchaguzi huo, ziligonga mwamba mara kadhaa.

Jumuiya ya kimataifa imekuwa ikitaka uchaguzi nchini humo kufanyika kama ilivyopangwa na hatima ya kisiasa nchini humo ipo kwenye njia panda baada ya maseneta kuonekana kuidhinisha mpango wa rais Farmajo kuongezewa muda wa kuendelea kuwa madarakani.