SOMALIA

Somalia: EU na Marekani zakosoa hatua ya rais Farmajo kuongezewa muda

Rais wa Somalia Mohamed Abdullahi Farmajo, february 8 2017.
Rais wa Somalia Mohamed Abdullahi Farmajo, february 8 2017. REUTERS/Feisal Omar

Umoja wa Ulaya na Marekani, zinasema zimesikitishwa na hatua ya wabunge nchini Somalia kumwongezea muda wa miaka miwili rais Mohamed Farmajo kuendelea kuwa madarakani.

Matangazo ya kibiashara

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Antony Blinken amesema hatua ya wabunge hao itasababisha vikwazo kutokana na kutowepo kwa mazungumzo ya kisiasa lakini pia kutishia usalama na amani ya nchi hiyo.

Wanasiasa wa upinzani nchini Somalia nao pia wamelaani hatua hiyo.

Juhudi za kutafuta mwafaka wa namna ya kufanikisha uchaguzi, zashindikana

Hatua ya wabunge nchini Somalia, imekuja baada ya serikali ya rais Farmajo kushindwa kuandaa uchaguzi mwezi Februari mwaka huu baada ya muda wake kumalizika.

Juhudi za kuwepo kwa maelewano kati ya wanasiasa nchini humo hasa kati ya uongozi wa Mogadishu na wakuu wa serikali ya serikali ya majimbo chini ya wawakilishi wa Umoja wa Mataifa, kutafuta mwafaka wa namna ya kufanikisha uchaguzi huo, ziligonga mwamba mara kadhaa.

Jumuiya ya kimataifa imekuwa ikitaka uchaguzi nchini humo kufanyika kama ilivyopangwa na hatima ya kisiasa nchini humo ipo kwenye njia panda baada ya maseneta kuonekana kuidhinisha mpango wa rais Farmajo kuongezewa muda wa kuendelea kuwa madarakani.