DRC

DRC: Ukosefu wa usalama waendelea kuripotiwa Shabunda, Kivu Kusini

Gari na askari wa kulinda amani nchini DRC,MONUSCO
Gari na askari wa kulinda amani nchini DRC,MONUSCO ONU

Tume ya Umoja wa Mataifa nchini DRC, MONUSCO, inasema ina wasiwasi juu ya kuendelea kwa ukosefu wa usalama huko Shabunda, eneo hili kubwa la mkoa wa Kivu Kusini, huku raia wakiangaishwa na hali hiyo na kulazimika kukimbilia katika maeneo salama.

Matangazo ya kibiashara

Ukosefu wa usalama unasababishwa hasa na makundi yenye silaha ambayo yameongeza mashambulizi yao dhidi ya raia, uporaji na unyanyasaji wa kijinsia katika eneo hili lenye msitu uliojaa madini. Moja ya vijiji vinavyokabiliwa hasa na ukosefu wa usalama ni Kigulube.

Katika kijiji hiki cha wakazi wapatao 4,000, wanawake na wasichana wadogo hasa wameelezea hali inayowakabili kwa tahadhari kwa sababu, mita chache kutoka kijiji hiki, wapiganaji wa Mai-Mai wamejificha msituni.

Dorika, 18, alibakwa miaka miwili iliyopita. "Nilikuwa mwanafunzi. Tukiwa njiani kuelekea shuleni na wenzangu, tuliingia kwenye mtegoo wa kundi la Raiya Mutomboki. Walinichukua kwa nguvu, walinibaka kabla ya kutuibia kila kitu. Baadaye nikagundua kuwa niko mjamzito. "

Visa vya unyanyasaji vyaripotiwa kwa wingi Shabunda

Kama vijiji vingine vingi, Kigulube ni kijiji kilichoathirika na mashambulio na unyanyasaji wa kijinsia uliofanywa kwanza na waasi wa Rwanda wa FDLR kati ya mwaka 1996 na 2010, halafu na makundi ya wanamgambo katika eneo hilo yanayojulikana kama "Raiya Mutomboki" baada ya kuondoka kwa FDLR. Tume ya Umoja wa Mataifa nchini DRC, MONUSCO inasema inatiwa wasiwasi na hali ya usalama ya sasa katika eneo la Shabunda, kulingana na Soro mkuu wa wa ofisi ya MONUSCO huko Bukavu.

"Hali bado ni mbaya mno katika eneo la Shabunda. Pia ni mahali ambapo makundi yenye silaha yanajihusisha na uporaji wa madini ambayo huwawezesha kupata uwezo wa kutekeleza uhalifu wao. Tuna karibu mitandao 20 ya tahadhari ya jamii katika eneo hili, na tunapokea kwa wastani tahadhari 20 (za unyanyasaji wa kijinsia) kwa wiki. Hivi karibuni, tahadhari zilikuwa nyingi sehemu ya Bamuguba Kaskazini mpakani na Kivu Kaskazini, na upande wa Kalole mpakani na Maniema, ”amesema.

MONUSCO kushirikiana na serikali kukabiliana na ukosefu wa usalama

Monusco anasema inafanya kazi kwa bidii na serikali za mitaa huko Kivu Kusini kurejesha mamlaka ya serikali huko Shabunda. Pamoja na hayo, mashirika ya kiraia katika kijiji cha Kigulube pia yameelezea masikitiko yao kutokana na hali mbaya ya barabara na hasa idadi ndogo ya wanajeshi kuimarisha usalama katika eneo hilo, na yametoa wito kwa serikali kushughulikia jambo hilo.