CHAD

Chad: jeshi latangaza kuwashikilia waasi kadhaa baada ya makabiliano makali

Sehemu ya jangwa la Chad karibu na Mao magharibi mwa Chad.
Sehemu ya jangwa la Chad karibu na Mao magharibi mwa Chad. AFP - PATRICK FORT

Chad inaendelea kushuhudia mdororo wa usalama, siku mbili baada ya mapigano makali kutokea kati ya vikosi vya serkali na waasi wa kundi la Front for Alternation and Concord in Chad (FACT) siku ya Jumamosi Aprili 17.

Matangazo ya kibiashara

Mapigano hayo yalitokea kaskazini mwa mji wa Mao, katika mkoa wa Kanem, zaidi ya kilomita 300 kutoka mji mkuu Ndjamena. Kundi la waasi wenye silaha, ambalo liliokea katika ngome yake kuu nchini Libya, liliingia nchini Chad Aprili 11 kwa lengo la kumtimua Idriss Deby mamlakani.

Waasi kadhaa wakamatwa

Jeshi limetangaza kati ya waasi 250 na 300 wameuawa, na waasi wengine 150 wamekamatwa ikiwa ni pamoja na kiongozi wa chama cha siasa ambaye aliamua kujiunga na kundi la waasi miaka michache iliyopita. Kundi lingine la waasi lilielekea upande wa magharibi na hadi jana jioni lilikuwa halijaonekana.

Waasi wa FACT walenga kuudhibiti mji mkuu N'Djamena

Siku ya Jumamosi, serikali ya Uingereza ilisema msafara wa FACT ulikuwa ukielekea kusini magharibi kuelekea mji mkuu N'Djamena na ulizidi mji wa Faya, kwenye umbali wa kilomita 770 (maili 478) na mji wa N'Djamena.

Msafara mwingine ulionekana ukikaribia mji wa Mao, karibu kilomita 220 kaskazini mwa N'Djamena, serikali ya Uingereza ilisema kwenye wavuti yake ya ushauri kwa kusafiri.

Hayo yanajiri wakati kulingana na matoko ya awali ya uchaguz, rais anaye maliza muda wake Idriss Deby Itno ameibuka mshindi katika uchaguzi wa urais uliofanyika Aprili 11.

Hata hivyo upinzani umesema kuwa hakuna uchaguzi uliofanyika nchini Chad. Viongozi wa upinzani walitoa wito kwa wafuasi wao kususia uchaguzi wa wiki iliyopita.