DRC- CHANJO

Chanjo aina ya AstraZeneca yaanza kutolewa nchini DRC

Chanjo aina ya Astra Zeneca iliyoanza kutolewa nchini DRC Aprili 19 2021
Chanjo aina ya Astra Zeneca iliyoanza kutolewa nchini DRC Aprili 19 2021 Gabriel Bouys AFP/Archivos

Serikali nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo,  imeanza kutoa chanjo aina ya AstraZeneca kwa raia wake, baada ya awali kuahirisha utoaji wa chanjo hiyo baada ya kupokea dozi Milioni 1.7 mwezi Machi.

Matangazo ya kibiashara

Timu iliyotumwa na ikulu ya raïs wa Jamhuri kupambana dhidi ya Covid-19 "iliamua chanjo zianze kutolewa siku ya  Jumatatu, kote nchini humo kwa mujibu wa Gilbert Kankonde, Waziri wa Mambo ya Ndani anayemaliza muda wake.

Chanjo itatolewa kwa hiari na kipaumbele ni kwa wahudumu wa afya, watu walio katika mazingira magumu wanaougua magonjwa ya kisukari na wote wanaofanya kazi katika mazingira magumu.

 Chanjo dhidi ya Covid 19 nchini DRC imekuwa ikizua maswali mengi huku baadhi ya watu wakidai hawaiamini.

Mimi sitapokea chanjo hiyo , hata familia yangu haitafanya hivyo. Naikataa. Amesema mkaazi mmoja wa jiji la Kinshasa.

Aidha, baadhi ya wakaazi wa Kinshasa wanataka viongozi wawe wa kwanza kupokea chanjo hiyo.

Mambo mengi yamesemwa kuhusu chanjo, wangeanza kwanza na raïs mwenyewe, kisha Magavana na viongozi wengine, lakini ninavyoona watu wengi hapa Kinshasa hawapo tayari.

Chanjo ilikuwa imepangwa kutolewa  tangu tarehe 15 mwezi Machi, lakini iliairishwa kama tahadhari" baada ya kusimamishwa na nchi zingine zilizokuwa zinatumia chanjo hiyo aina ya  AstraZeneca baada ya kuwepo kwa visa vya kuganda kwa damu mwilini.

Tangu kutangazwa kwa janga la Covid 19  tarehe 10 Machi mwaka 2020, DRC imerikodi kesi zaidi ya 28,000 na vifo zaidi ya 700.

Kati ya majimbo ishirini na sita nchini humo ni majimbo 23 ndio yaliyoathiriwa huku jiji kuu Kinshasa likiathiriwa zaidi.