CHAD - SIASA

Rais wa Chad Idriss Deby auawa baada ya kushambuliwa na wanajihadi

Rais wa Chad Idriss Deby, ambaye amefariki leo
Rais wa Chad Idriss Deby, ambaye amefariki leo AFP - MARCO LONGARI

Rais wa Chad Idriss Déby ameuawa baada ya makabiliano na waasi Kaskazini mwa nchi hiyo mwishoni mwa wiki iliyopita karibu na mpaka wa Libya.

Matangazo ya kibiashara

Jeshi nchini humo kupitia Televisheni ya Taifa, limetangaza kifo cha Deby aliyejeruhiwa katika makabiliano hayo baada ya kulitembelea jeshi la taifa lake lililokuwa linakabiliana na waasi wanaojiita The Front for Change and Concord in Chad, FACT.

Kupitia taarifa msemaji wa jeshi Jenerali Azem Bermandoa Agouna amesema

Ameuawa  akipigania usalama wa taifa letu, mwishoni mwa juma

Deby mwenye Umri wa miaka 68, ameuawa  baada ya kushinda uchaguzi kuongoza taifa hilo kwa muhula wa sita katika uchaguzi ambao upinzani ulisusia.

Kiongozi wa kundi hilo la kijihadi FACT, Mahamat Mahdi Ali amekiri kundi lake kuhusika na mauaji ya kiongozi huyo wa Chad.

Alifikiri hawezi kuguswa. Alidanganywa na Majenerali wake akaja kwenye mapambano ya vita.Alipokuja tulimshambulia na akajeruhiwa, aakasafirishwa kwa helikopta. Alikuwa katika mstari wa mbele, kama kiongozi wa kijeshi, tukamwona anapigana tukafahamu kuwa yupo hapo.

Kufuatia kifo cha rais Deby, serikali na bunge zimevunjwa na Baraza la Jeshi litaongoza kwa muda wa miezi 18 ijayo.

Mipaka ya nchi hiyo imefungwa huku hali ya watu kutotembea nje ikitangazwa kati ya saa 12 jioni mpaka saa 11 Alfajiri.

Aidha, Jeshi nchini humo limetangaza kuwa Jenerali Mahamat Kaka, mtoto wa kiume wa Marehemu Deby ndiye atakayeongoza baraza hilo la jeshi.