DRC-KENYA

Kenya na DRC zakubaliana kushirikiana kwenye masuala ya usalama na biashara

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta (Kushoto) akiwa na mwenyeji wake Felix Thisekedi baada ya kuwasili jijini Kinshasa Aprili 20 2021
Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta (Kushoto) akiwa na mwenyeji wake Felix Thisekedi baada ya kuwasili jijini Kinshasa Aprili 20 2021 © StateHouseKenya

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta anazuru nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kwa ziara ya siku tatu kutiliana saini mikataba na mwenyeji wake Felix Thisekedi, ili kuimarisha uchumi na mahusiano kati ya nchi hizo mbili.

Matangazo ya kibiashara

Wakuu wa nchi hizo mbili wamekubaliana kushirikiana  zaidi katika masuala ya  usalama hasa vita dhidi ya ugaidi, biashara na  diplomasia kuimarisha mahusiano ya watu wa mataifa hayo mawili.

Changamoto za usalama nchini DRC hasa Mashariki mwa nchi hiyo kwa muda mrefu, zimesababisha hofu kwa wafanyibiashara wa Kenya kuja kuwekeza lakini tangu mwaka 2014 mambo yameanza kubadilika na wawekezaji kutoka Kenya wameanza kuwekeza nchini humo ikiwemo kufungua Benki.

Ziara hii ya rais Kenyatta imekuja wakati huu ikiendelea kupata ushindani kutoka kwa Tanzania kuhusu matumizi ya bandari ya Dar es salaam na Mombasa zinazotumiwa na nchi hiyo kuingiza bidhaa mbalimbali.

Kuimarisha biashara kati ya nchi hizo mbili, Kenya inafungua ubalozi mdogo mjini Goma katika jimbo la Kivu Kaskazini na kuwa na wawakilishi mjini Lubumbashi na Kivu Kusini.

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ambayo imeomba kujiunga na Jumuiya ya Afrika Mashariki, Jumuiya ambayo kwa sasa rais Uhuru Kenyatta ndiye Mwenyekiti.