Vita DRC: Kinshasa na Kampala watofautiana kuhusu malipo ya fidia

Mahakama ya Haki ya Kimataifa (ICJ ) huko Hague, Uholanzi (picha ya kumbukumbu)
Mahakama ya Haki ya Kimataifa (ICJ ) huko Hague, Uholanzi (picha ya kumbukumbu) AP - Peter Dejong

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Uganda zinaendelea kukabiliana kwa siku zaidi ya kumi mbele ya Mahakama Kuu ya Haki ya Kimataifa, International Court of Justice (ICJ).

Matangazo ya kibiashara

Mwaka 2005, mahakama hii ya Umoja wa mataifa ilitangaza Uganda kuwa na hatia ya kuingilia katika masuala ya ndani mashariki mwa DRC, eneo lilikuwa chini ya udhibiti wa majeshi ya Uganda kati ya mwaka 1998 na 2003.

Kinshasa na Kampala walitakiwa kukubaliana juu ya kiwango cha fedha kuhusiana na fidia  ambayo Uganda inatakiwa kulipa, lakini miaka kumi na tano hakutosha. Kwa kukosekana kwa makubaliano, DRC iliwasilisha tena malalamiko yake mbele ya Mahakama ya Kimataifa ya Haki. Mbele ya majaji wake 15, mwanadiplomasia Paul Crispin Kakhozi Bin Bulongo amekumbusha ukubwa wa uhalifu huo.

Vita mashariki mwa DRC vyasababisha vifo vya watu 400,000

Hasara iliyopata nchi yangu kutokana na vitendo vya Uganda ni kubwa zaidi. Vitendo visivyo halali vilivyofanywa na Uganda dhidi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo vimepoteza maisha ya wanajeshi wetu wengi, vimeathiri sana miundombinu na mazingira, viliumiza raia wa taifa hili, na kutokomeza uchumi wa DRC.

Majaji waliliweka hatiani jeshi la Uganda na wanamgambo wake wasaidizi kwa mateso, mauaji, uharibifu, uporaji na utumiaji haramu wa maliasili ya mkoa tajiri wa Ituri.

Uganda yafutilia mbali madai ya DRC

DRC inadai zaidi ya dola bilioni 13. Kinshasa inakadiria kuwa kutokana na Uganda pekee, watu 400,000 walipoteza maisha, visa 1,730 vya ubakaji viliripotiwa, watoto 2,500 waliajiriwa katika jeshi la Uganda, na raia 600,000 waliyatoroka makazi yao.

Hata hivyo Uganda inafutilia mbali madai hayo ya DRC na kutokubaliana kiwango cha fedha kama fidia.

Kampala itajibu maombi ya DRC Alhamisi. Ili kuweza kutathmini uharibifu uliofanywa mashariki mwa DRC, majaji wa ICJ watajikita na ripoti za wataalam wanne, ambao watasikilizwa katika siku zijazo.