DRC-USALAMA

Rais Tshisekedi atangaza hatua za kukabiliana na utovu wa usalama Mashariki kwa DRC

Wanajeshi wa Umoja wa Mataifa MONUSCO wakipiga doria katika mji wa Djugu mkoani Ituri Mashariki mwa DRC
Wanajeshi wa Umoja wa Mataifa MONUSCO wakipiga doria katika mji wa Djugu mkoani Ituri Mashariki mwa DRC AFP/Archivos

Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Felix Tshisekedi , imetangaza kufungwa kwa majimbo mawili Mashariki mwa nchi hiyo, kufuatia ongezeko la utovu wa usalama unaosabishwa na makundi yenye silaha kuwauwa raia.

Matangazo ya kibiashara

Msemaji wa serikali Patrick Muyaya ametangaza hatua hii kwa niaba ya rais Tshisekedi  ambaye amelieleza Baraza la Mawaziri kuwa hatua hii imekuja kutokana na utovu wa usalama katika mikoa ya Ituri na Kivu Kaskazini.

Hata hivyo, hatua zilizochukuliwa hazijawekwa wazi lakini ripoti zinasema kuwa, zitawekwa bayana saa chache  zijazo.

Katiba ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, inampa mamlaka rais kutangaza hali ya hatari iwapo kuna jambo ambalo linatishia usalama wa nchi hiyo.

Hatua hii imekuja  baada ya rais Tshisekedi  siku ya Alhamisi kutangaza kuwa, alikuwa anaanda mikakati ya kukabiliana na utovu wa usalama Mashariki mwa nchi hiyo, huku akiiomba Ufaransa kuisaidia.

Tangu miaka ya tisini, kumeripotiwa makundi ya waasi 122 yanayoenendelea kusababisha mauaji ya maelfu ya raia na mamilioni kuyakimbia makwao katika eneo hilo la Mashariki mwa DRC.