DRC

DRC: Mtu mmoja afariki dunia wakati wa sala ya Eid al Fitr Kinshasa

Gari la polisi limechomwa moto baada ya makabiliano kati ya Waislamu na polisi wakati wa kumalizika kwa sala ya Eid al Fitr huko Kinshasa, Mei 13, 2021.
Gari la polisi limechomwa moto baada ya makabiliano kati ya Waislamu na polisi wakati wa kumalizika kwa sala ya Eid al Fitr huko Kinshasa, Mei 13, 2021. © Pascal Mulegwa/RFI

Vurugu zilizuka mjini Kinshasa katika uwanja wa Mashujaa (Martyrs) Alhamisi  hii, Mei 13, ambapo sala kuu ya Eid al-Fitr ya kumalizia mfungo wa Ramadhan ilifanyika. Waumini kadhaa wa dini ya Uislamu walikabiliana na vikosi vya usalama  na kusababisha kifo cha afisa mmoja wa polisi na wengine wengi kujeruhiwa, kulingana na polisi.

Matangazo ya kibiashara

Vurugu zilisababisha mgawanyiko ndani ya jamii ya Waislamu katika nchi hii yenye Wakristo wengi. Angalau polisi mmoja ameuawa, gari moja ya vikosi vya usalama ilichomwa moto na watu kadhaa wamekamatwa. Vurugu zilianza kabla ya kuanza kwa sala takatifu ya Eid al Fitr.

Mvutano katika jamii ya Waislamu jijini KInshasa ulitabiriwa tangu mapema na polisi imekuwa imejiandaa mapema asubuhi kwa kupeleka karibu na Uwanja wa Martyrs maafisa wake.

Kama ilivyoamuliwa siku moja kabla na gavana wa Kinshasa, sala hiyo ilikuwa iongozwe na mwakilishi rasmi wa jumuiya ya Waislamu nchini DRC, Sheikh Adballah Mangala na Youssouf Djibondo amekuwa akipinga uhalali wake kwa miezi kadhaa. Kesi iko mbele ya mahakama. Kulingana na mashuhuda, baadhi ya waumini walitaka kumshambulia Sheikh Abdullah Mangala, hali ambayo ilipelekea polisi kuingilia kati.

Kulingana na mkuu wa polisi katika mji wa Kinshasa Sylvano Kasongo, afisa mmoja wa polisi aliuawa kwa kupigwa mawe na baadhi ya waumini wa Kiislamu, maafisa 46 wa polisi wamejeruhiwa, gari moja la polisi lilichomwa moto, magari kadhaa ya raia yalichomwa moto na watu 30 wamekamatwa.

Makundi mawili katika jumuiya ya Waislamu nchini DRC yanadai kwamba mbali na afisa wa polisi aliyeuawa, Waumini wawili wameuawa kwa kupigwa risasi. Taarifa ambayo RFI haijaweza kuthibitisha kutoka kwa chanzo huru.