AFRIKA-UFARANSA

Mkutano wa Paris: Emmanuel Macron azitaka nchi tajiri kusaidia uchumi wa Afrika

Rais wa Ufaransa, mwenyeji wa mkutano wa kilele wa Paris kuhusu ufadhili wa uchumi wa Afrika, akisalimiana na Rais wa Comoro Azali Assoumani (kushoto) na Rais wa Nigeria Muhammadu Buhari, Mei 18, 2021
Rais wa Ufaransa, mwenyeji wa mkutano wa kilele wa Paris kuhusu ufadhili wa uchumi wa Afrika, akisalimiana na Rais wa Comoro Azali Assoumani (kushoto) na Rais wa Nigeria Muhammadu Buhari, Mei 18, 2021 REUTERS - POOL

Janga la COVID-19 limeathiri  bara la Afrika kwa kudorora kwa uchumi wake. Nchi za Kiafrika zinahitaji kuinua uchumi wao, lakini tofauti na nchi zenye nguvu, hazina uwezo sawa. Mkutano wa kilele wa Paris uliolenga kufufua uchumi dhaifu, suala la deni na mgogoro wa kiafya ulimalizika Jumanne hii jioni.

Matangazo ya kibiashara

Mkutano na waandishi wa habari ulianza kabla ya saa 2:30 usiku, baada ya zaidi ya saa tano ya mkutano. Emmanuel Macron alikuwa wa kwanza kuzungumza. Rais wa Ufaransa alirejelea malengo ya mkutano huo: kutoa majibu kwa muda mfupi na kuzindua malengo katika kufufua uchumi wa Afrika. Matarajio yalikuwa kukusanya dola bilioni 100, aliahidi kufanikisha. "Tumeweza kusonga mbele," alisisitiza Emmanuel Macron ingawa anakubali kuwa sio kila kitu kinaweza kurekebishwa mara moja.

Licha ya kutoathirika pakubwa na janga la Corona, kama ilivyo katika mataifa ya mengine duniani, uchumi wa mataifa hayo umeyumba huku idadi kubwa ya watu wakipoteza ajira.

Shirika la fedha duniani IMF limeonya kuwa mataifa ya Afrika, yanahitaji msaada wa kifedha kwa ajili ya miradi ya maendeleo na angalau dola Bilioni 290 zinahitajika kufikia mwaka 2023.

Mkutano huu umekuja siku moja baada ya rais Macron na viongozi hao wa Afrika kukutana kwa ajili ya kuisaidia nchi ya Sudan ambayo kwa sasa inaongozwa na serikali ya mpito chini ya Waziri Mkuu Abdalla Hamdok.

Katika mkutano huo, Macron alitangaza kuwa nchi yake inafuta deni la Dola Bilioni tano, iliyokuwa inaidai Sudan.

Wakati mkutano huu ukifanyika, bara la Afrika limeshuhudoa maambukizi ya Corona, changamoto kubwa ikiwa ni upatikanaji wa chanjo, katika bara hilo ambalo limewapoteza watu 130,000 kutokana na virusi hivyo.