SOMALIA-SIASA

Somalia: Wanasiasa na jumuiya ya kimataifa kujadili kalenda ya uchaguzi

Somalia inaendelea kuathirika kutokana na mizozo ya kisiasa isiyoisha.
Somalia inaendelea kuathirika kutokana na mizozo ya kisiasa isiyoisha. REUTERS - FEISAL OMAR

Viongozi wa siasa nchini Somalia na wawakilishi kutoka Jumuiya ya Kimataifa wanatarajiwa kukutana Jumamosi wiki hii mjini Mogadishu, kujadiliana kuhusu kalenda ya kufanyika kwa Uchaguzi nchini humo.

Matangazo ya kibiashara

Waziri Mkuu Mohamed Hussein Roble ndiye atakayeongoza mazungumzo hayo, kuona iwapo viongozi nchini humo watakubaliana kuhusu mfumo gani utumike kumchagua kiongozi wa nchi hiyo.

Uchaguzi nchini Somalia ulikuwa umepangwa kufanyika mwezi Februari, lakini haikuwa hivyo baada ya wanasiasa kushindwa kuelewana kuhusu mfumo wa uchaguzi huo.

Hatua ya kutofanya uchaguzi imeiweka Somalia katika hali tete kisiasa, mnamo wakati nchi hiyo inakabiliwa na ongezeko la mashambulizi ya wanamgambo, uvamizi wa nzige na uhaba wa chakula.

Farmajo ambaye anawania muhula wake wa pili anawashutumu wapinzani wake kwa kutotekeleza makubaliano ya awali ya mwezi Septemba, ambayo yaliainisha tarehe ya uchaguzi.

Kulingana na makubaliano hayo, uchaguzi wa bunge ungefanyika mwezi Desemba mwaka 2020 na wa rais ungefanyika mapema mwaka 2021.