NIGERIA-AJALI

Ajali ya ndege yasababisha kifo cha Mkuu wa Majeshi nchini Nigeria

Aliyekuwa Mkuu wa Majeshi nchini Nigeria Marehemu  Ibrahim Attahiru aliyapata ajali ya ndege na kupoteza maisha Mei 21 2021
Aliyekuwa Mkuu wa Majeshi nchini Nigeria Marehemu Ibrahim Attahiru aliyapata ajali ya ndege na kupoteza maisha Mei 21 2021 © Audu Marte AFP/Archivos

Mkuu wa Majeshi nchini Nigeria, Luteni Jenerali Ibrahim Attahiru, na maafisa wengine 10 waliopoteza maisha jana baada ya ndege yao kuanguka katika jimbo la Kaduna siku ya Ijumaa, wamezikwa kwenye makaburi ya kijeshi jijini Abuja.

Matangazo ya kibiashara

Ndege iliyokuwa imembeba Mkuu huyo wa Majeshi, ilianguka wakati ikijaribu kutua kwa sababu ya hali mbaya ya hewa katika uwanja wa Kimataufa wa ndege wa Kaduna.

Mbali na Luteni Jenerali Ibrahim Attahiru, ndege hiyo ilikuwa na maafisa wengine 10 wa kijeshi na wahudumu wa ndege ambao pia wote walipoteza maisha.

Rais Muhammadu Buhari amesema amesikitishwa na kifo cha mkuu huyo wa majeshi, ambaye alimteua katika nafasi hiyo mwezi Januari.

Jenerali Attahiru mwenye umri wa miaka 54, aliteuliwa na rais Buhari miezi minne iliyopita kufuatia mabadiliko katika uongozi wa jeshi ili kuendeleza mapambano dhidi ya kundi la kijihadi la Boko Haram.

Jeshi la Nigeria limeapa kuendelea kukabiliana na changamoto za kiusalama hasa mapambano dhidi ya kundi la Boko Haram, Kaskazini mwa nchi hiyo.

Nigeria imekuwa ikiendeleza mapambano dhidi ya kundi la Boko Haram tangu mwaka 2009, kundi ambalo limesababisha vifo vya watu 40,000 na kuwaacha wengine zaidi ya Milioni mbili bila makaazi.