DRC

Mlipuko wa Nyiragongo DRC: Wakazi wa Buhene bado wana kiwewe

Mji wa Goma na viunga vyake, Mei 2021.
Mji wa Goma na viunga vyake, Mei 2021. AFP - JUSTIN KATUMWA

Mtetemleko wa ardhi umesikika tena Jumatatu hii asubuhi , Mei 24 katika mji wa Goma, mji mkuu wa mkoa wa Kivu Kaskazini, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Matangazo ya kibiashara

Mitetemeko ya ardhi inayotokana na volkano imeendelea kuzua wasiwasi kwa wakazi wa mji mkuu wa Kivu Kaskazini, baada ya Jumamosi jioni kutokea mlipuko wa volkano ya Niyragongo. Kufikia sasa, kulingana na vyanzo mbalimbali kutoka Goma, watu zaidi ya ishirini walipoteza maisha kufuatia mlipiko huo. Maeneo kadhaa pembezoni mwa mji wa Goma yameharibiwa na tope la volkano, hasa eneo la Buhene.

Wakazi kadhaa walijikuta nyumba zao ziliathirika kabisa baada ya kuvamiwa na tope la volkano Jumamosi jioni hadi Jumapili asubuhi, kulingana na mwandishi wetu katika eneo hilo, William Basimike, huku wengine wakiwapoteza ndugu zao.

Raia wanaoma serikali iwasaidie, kwani kwa sasa hawana cha kufanya.

Floribert Chumba ni mmoja wa watu waliopoteza mali zao na bado anatafuta mabaki ya watoto zake wawili ambao anaamini walifunikwa na tope la volkano. Amekuwa anawatafuta katika mabaki ya nyumba ya jirani yake: “Hii ilikuwa nyumba yangu. Nyumba zote hazionekani tena. Hatuna chochote kilichobaki. Tunaomba serikali itusaidie, kwa sababu hatuna kitu kingine cha kufanya. Nilipoteza mbuzi wangu na vifaa vingine vya nyumbani. "

Athari zingine zaanza kujitokeza baada ya mlipuko wa volkano Nyiragongo

Wakazi wa maeneo yaliyoathiriwa wana hofu ya kupoteza maisha kutokana na harufu ya moshi kutoka kwenye tope la Volkano.

Mtu mmoja amefariki dunia leo Jumatatu asubuhi katika eneo la Buhene baada ya kuvuta harufu ya moshi huo, amebaini jirani yake Bakanga Samuel.

"Tumemkuta amelala chini, baada ya kuingia chooni na kuvuta moshi uliokuwa ukitokea kwenye tundu la choo. Tunaamini kuwa harufu ya moshi huo ndio ulimuua", amesema.

Watu wengine wawili walifariki dunia usiku wa Jumapili kuamkia Jumatatu hii katika eneo la Kibati, kaskazini mwa Goma baada ay kuvuta harufu ya moshi wa tope la volkano. Kutokana na hali hiyo shule na vyuo vikuu vimeamua kufungwa.