ETHIOPIA-USALAMA

Mzozo Tigray: Marekani yaziwekea vikwazo Ethiopia na Eritrea

Wakazi wa Tigray wamewahusisha wanajeshi wa Ethiopia na Eritrea mauaji ya watu kadhaa katika miji kama Dengolat.
Wakazi wa Tigray wamewahusisha wanajeshi wa Ethiopia na Eritrea mauaji ya watu kadhaa katika miji kama Dengolat. EDUARDO SOTERAS AFP/File

Marekani imetangaza vikwazo vya viza kwa maafisa wa serikali nchini Ethiopia na Eritrea kwa kuchochea mzozo katika jimbo la Tigray nchini Ethiopia ambao umeendelea kwa mwezi wa sita sasa.

Matangazo ya kibiashara

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken katika taarifa yake amesema kuwa hatua hyo imechukuliwa kwa sababu maafisa wa nchi hizo mbili, hawajachukua hatua yoyote kumaliza mzozo huo.

Waliolengwa katika vikwazo hivyo ni maafisa wa sasa na wa zamani wa nchi hizo mbili, viongzi wa usalama, pamoja na viongozi kutoka jimbo la Amhara na wapiganaji wa TPLF katika jimbo la Tigray.

Aidha, Blinken ametangaza kusitisha ushirikiano wa kiuchumi na usalama kati ya Marekani na Ethiopia, lakini itaendelea kutoa msaada wa kibinadamu kama chakula, dawa na elimu kwa wananchi wenye uhitaji.

Mzozo wa jimbo la Tigray ulizuka mapema mwezi Novemba mwaka uliopita, baada ya vikosi vya Ethiopia kuanza makabiliano na vikosi vya TPLF.

Mashirika ya kimataigfa yamelishtumu majeshi ya Ethiopia na Eritrea kwa kusababisha maafa makubwa ya raia na kusababisha maelfu ya watu wengine kuyakimbia makwao katika jimbo hilo la Tigray.