MALI-SIASA

Mali: Kanali Assimi Goïta atangazwa rais wa mpito

Makamu wa rais Assimi Goita wakati wa mkutano wa ECOWAS huko Accra, Septemba 15, 2020.
Makamu wa rais Assimi Goita wakati wa mkutano wa ECOWAS huko Accra, Septemba 15, 2020. Nipah Dennis / AFP

Mahakama ya Katiba nchini Mali imemtangaza Assimi Goïta, afisa wa jeshi mwenye cheo cha kanali ambaye, kama makamu wa rais wa Mali, aliwafuta kazi rais Bah Ndaw na Waziri Mkuu Moctar Ouane wiki hii na kujitangaza rais mpya wa mpito.

Matangazo ya kibiashara

Bah Ndaw na Moctar Ouane waliachiliwa baada ya kujiuzulu siku mbili baada ya kukamatwa na jeshi.

Uamuzi wa Mahakama ya Katiba nchini Mali inasema kwamba makamu wa rais wa mpito, Kanali Goïta, "anatumia majukumu, sifa na haki za rais wa mpito kuongoza kipindi cha mpito kufikia mwisho wake", na kwamba atachukua " nafasi na kuitwa rais wa mpito, mkuu wa nchi ". Mahakama ya Katiba imetoa uamuzi huo baada ya kubaini kuwa "nafasi ya rais iko wazi" kufuatia kujiuzulu kwa Bah N'Daw, ambaye hadi wakati huo alikuwa rais wa mpito.

Siku ya Ijumaa Assimi Goïta pia alikutana kwa mara ya kwanza na wanasiasa mbalimbali nchini Mali. Alianza kwa kutetea mapinduzi ya hivi karibuni kabla ya kuanza mkutano huo, ameripoti mwandishi wetu huko Bamako, Serge Daniel.

"Sote tumechukuwa hatua kwa masilahi makubwa ya taifa," Kanali Goïta alihakikisha. Tulilazimika kuchagua kati ya utulivu wa Mali na machafuko. Tulichagua utulivu. Leo, kuna maswala mengi kuhusu Mali, ndiyo sababu tunahitaji umoja, tunahitaji kushikamana ili kulinda maslahi makubwa ya taifa. Hatuna chaguo lingine ”.

Goita alikuwa makamu wa rais baada ya kuongoza mapinduzi mwezi Agosti mwaka uliopita na kumuondoa madarakani Rais Ibrahim Boubacar Keita. Ndaw na Waziri Mkuu, Moctar Ouane ambao walishikiliwa baada ya mapinduzi hayo walijiuzulu siku ya Jumatano, wakiwa bado kizuizini. Viongozi hao waliokuwa katika serikali ya mpito waliachiwa huru siku ya Alhamisi. Hayo ni mapinduzi ya pili kufanyika Mali ndani ya kipindi cha mwaka mmoja.