DRC-USALAMA

Ripoti: Watu 50 wauawa katika mashambulio nchini DRC

Hali inayowakumba wakaazi wa mashariki mwa DRC, filamu iliyochezwa kuonyesha madhila wanayokabiliana nayo raia wa DRC, mashariki mwa nchi.
Hali inayowakumba wakaazi wa mashariki mwa DRC, filamu iliyochezwa kuonyesha madhila wanayokabiliana nayo raia wa DRC, mashariki mwa nchi. © Reuters

Watu wasiopungua 50 waliuawa Jumapili usiku katika mashambulio mawili kwenye vijiji kadhaa, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) katika kile kinachoweza kuwa usiku mbaya zaidi wa vurugu katika mkoa huo kuwahi kutokea kwa angalau miaka minne, kundi linalojihusisha na Usalama katikaeneo la Kivu (KST) limesema Jumatatu wiki hii.

Matangazo ya kibiashara

Jeshi na kundi la kutetea haki za binadamu wameshutumu kundi la waasi wa Allied Democratic Forces (FDA), kundi la wanamgambo wa kiislamu lililoko Uganda, kwa kushambulia kijiji cha Tchabi na kambi ya wakimbizi wa ndani karibu na kijiji cha Boga.

Maeneo hayo mawili yako karibu na mpaka na Uganda.

Albert Basegu, mkuu wa shirika la kutetea haki za binadamu huko Boga, ameliambia kwa njia ya simu shirika la habari la REUTERS kwamba aliarifiwa juu ya shambulio hilo kwa kelele kutoka kwa jirani yake.

"Nilipofika katika eneo la shambulio, niligundua kuwa washambuliaji walikuwa tayari wamemuua mchungaji wa kanisa la Anglikana na kwamba binti yake pia alijeruhiwa vibaya," amesema.

KST, ambayo imekuwa ikiratibu machafuko mashariki mwa DRC tangu mwezi Juni 2017, imeandika kwenye Twitter kwamba watu 28 waliuawa huko Boga na 22 huko Tchabi.

Marekani yaita FDA kundi la kigaidi

"Miongoni mwa waathiriwa wa shambulio la Tchabi ni mke wa mkuu eneo la Banyali-Tchabi", linabainisha kundi hili la watafiti, likisema kuwa ni idadi kubwa zaidi ya vifo kuwahi kurekodiwa na KST kwa siku moja.

Kulingana na Umoja wa Mataifa, FDA iliua zaidi ya watu 850 mnamo mwaka 2020, wakati wa kulipiza kisasi dhidi ya raia baada ya operesheni za kijeshi dhidi ya kundi hilo mwaka uliopita.

Mwezi Machi mwaka huu, Marekani iliita kundi la FDA kama kundi la kigaidi kutoka ugenini.

Kundi hilo hapo awali lilitangaza kuwa na mafungamano na kundi la Islamic State, ingawa Umoja wa Mataifa unasema ushahidi unaoonyesha uhusiano wa kundi hilo na mitandao mingine ya Kiisilamu ni adimu.