ETHIOPIA

WFP yaonya kuhusu uhaba wa chakula unaowakabili wakazi wa Tigray

Wakimbizi wa Ethiopia wanaokimbia mapigano katika mkoa wa Tigray, wanasubiri chakula katika kambi ya Umoja wa Mataifa ya Rakoba, mpakani mwa Sudan na Ethiopia, katika jimbo la al-Qadarif, Sudan Novemba 23, 2020.
Wakimbizi wa Ethiopia wanaokimbia mapigano katika mkoa wa Tigray, wanasubiri chakula katika kambi ya Umoja wa Mataifa ya Rakoba, mpakani mwa Sudan na Ethiopia, katika jimbo la al-Qadarif, Sudan Novemba 23, 2020. REUTERS - MOHAMED NURELDIN ABDALLAH

Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula duniani, WFP, linasema viwango vya njaa vinaongezeka katika eneo la kaskazini mwa Ethiopia wakati shirika hilo likihitaji  Dola za Marekani Milioni 203 ili kukidhi mahitaji ya sasa.

Matangazo ya kibiashara

Umoja wa Mataifa umeonya kuwa Jumla ya watu milioni 5.2 katika eneo la Tigray lililokumbwa na vita nchini Ethiopia, au asilimia 91 ya wakazi wake, wanahitaji msaada wa chakula wa dharura. Onyo hilo la shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) limekuja wakati ikiomba zaidi ya dola Milioni 200 kuongeza majibu yake katika mkoa wa kaskazini ambapo karibu miezi saba ya mapigano yamesababisha tayari ongezeko la viwango vya njaa.

WFP inasema inastaajabishwa na athari za mzozo kwa kiwango kikubwa cha njaa, ambapo msemaji wake Tomson Phiri aliwaambia waandishi wa habari huko Geneva kwamba wanatiwa wasiwasi sana na idadi ya watu wanaonekana kuwa na mahitaji ya msaada wa lishe na msaada wa chakula cha dharura.

WFP yasadia watu zaidi ya Milioni 1

Shirika hilo limesema limetoa msaada wa dharura kwa zaidi ya watu Milioni moja tangu ilipoanza usambazaji katika maeneo ya kaskazini magharibi na kusini mwa jimbo la Tigray mwezi Machi.

WFP inataka dola Milioni 203 kuendelea kuongeza jibu lake huko Tigray kuokoa maisha ya watu hadi mwisho wa mwaka.

Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed, mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel ya mwaka 2019, aliamuru operesheni ya kijeshi ya ardhini na angani huko Tigray mapema Novemba 2020 baada ya kukituhumu chama kilichokuwa kikitawala eneo hilo kaskazini, Tigray People's Liberation Front (TPLF), kwa kupanga mashambulizi dhidi ya kambi za jeshi la shirikisho.