DRC-USALAMA

Tisa waangamia katika shambulizi la ADF Mashariki mwa DRC

Maafisa wa usalama wakiwa Ituri, Mashariki mwa DRC
Maafisa wa usalama wakiwa Ituri, Mashariki mwa DRC SAMIR TOUNSI / AFP

Watu tisa wameuawa katika shambulizi jipya linalodaiwa kutekelezwa na waasi wa ADF katika mkoa wa Kivu Kaskazini na Ituri, Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Matangazo ya kibiashara

Ripoti zinasema, mashambulizi ya hivi punde yamekuwa yakiwamenga wakulima wanaoishi katika mpaka wa Ituri na mkoa wa Kivu Kaskazini.

Mkuu wa Wilaya ya Beni Donat Kibwana ameliambia Shirika la Habari la Ufaransa AFP kuwa, milli hiyo imepelekwa katika chumba cha kuhifadhi maiti katika mji wa Oicha.

Lewis Saliboko kiongozi wa Shirika la kiraia amesema watu waliouawa walichomwa visu na wengine walikuwa wamekatwa vichwa.

Ripoti zingine zinaeleza kuwa, miili ya watu wengine 13 ilipatikana msituni, na kufikisha idadi ya watu waliouawa kufikia 22 kwa mujibu wa wahudumu wa afya.

Tangu mwaka uliopita, kundi la ADF linadaiwa kuwauwa mamia ya raia, Mashariki mwa nchi hiyo na mauaji haya yanaendelea wakati huu, mikoa ya Kivu Kaskazini na Ituri ikiwa chini ya uongozi wa kijeshi.