DRC-USALAMA

DRC: Kiongozi wa kivita katika Hifadhi ya Virunga akamatwa

Walinda mazingira katika Hifadhi ya Virunga wakipiga doria. (picha ya kumbukumbu)
Walinda mazingira katika Hifadhi ya Virunga wakipiga doria. (picha ya kumbukumbu) Virunga National Park/AFP/File

Mbabe wa kivita anayeshukiwa kuua walinda mazingira karibu 20 katika Hifadhi ya Kitaifa ya Virunga anashikiliwa na idara za usalama katika mkoa wa Kivu Kaskazini, ulio chini ya sheria za kijeshi. Jackson Muhukambuto pia anasemekana kuwa mwindaji haramu anayefanya biashara ya meno ya tembo.

Matangazo ya kibiashara

Jackson Muhukambuto alikamatwa mapema wiki hii nje kidogo ya mji wa Butembo. Ilichukuwa miezi sita ili Walinzi wa mazingira wafanikiwe kumkamata, amesema mkurugenzi wa Hifadhi ya Kitaifa ya Virunga. Kulingana na Emmanuel de Merode, Jackson Muhukambuto na kundi lake la wanamgambo, Mai Mai Jackson, wanashukiwa kuhusika katika mauaji kadhaa.

Katika kipindi cha miaka mitatu, inasemekana waliwaua walinzi wa mazingira kumi na tisa, raia wengi pamoja na wanajeshi kadhaa.

Jackson Muhukambuto ambaye ni mto katika jeshi la FARDC na mpiganaji wa zamani katika makundi kadhaa ya waasi, anaongoza kundi lenye silaha linalotekeleza uhalifu wake katika eneo linalokadiriwa kuwa zaidi ya nusu ya Hifadhii ya Virunga. Hifadhi inayopima kilomita mraba 7,800.

Jackson Muhukambuto anasemekana kuwa na mitandao yenye nguvu ndani ya jeshi na kati ya wafanyabiashara katika jamii ya Nande, ripoti ya hivi karibuni kuhusu hali ya makundi yenye silaha mashariki mwa DRC ilisema.

Kulingana na vyanzo vya kutokaHifadhi ya Viunga, kukamatwa kwa Muhukambuto kulikuja baada ya kurushiana risasi kati ya wapiganaji wake na walinzi wa mazingira.