UFARANSA-SAHEL

Sahel: Ufaransa yataka kubadilisha mfumo na mkakati katika vita dhidi ya ugaidi

Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa ametangaza kwamba operesheni za kijeshi za taifa hilo katika mapambano dhidi ya wanamgambo walio na itikadi kali katika ukanda wa Sahel zinafikia mwisho.
Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa ametangaza kwamba operesheni za kijeshi za taifa hilo katika mapambano dhidi ya wanamgambo walio na itikadi kali katika ukanda wa Sahel zinafikia mwisho. AP - Christophe Petit Tesson

Rais Macron anataka "kubadilisha" kwa kina uwepo wa jeshi la Ufaransa katika ukanda wa Sahel. Ameyasema hayo katika mkutano na waandishi wa habari Alhamisi jioni.

Matangazo ya kibiashara

Kwa kweli, hii inamaanisha kupunguzwa kwa wanajeshi wa Ufaransa katika eneo hilo, na "mwisho wa Operesheni Barkhane kama operesheni ya nje ya nchi", kwa faida ya muungano wa kimataifa unaoleta pamoja mataifa ya ukanda huo na Ulaya.

"Mfumo huu wa kuwepo kwetu" huko Sahel "hauendani tena na hali halisi ya mapigano," Rais Macron alisema. Kwa kweli, tangazo lililotolewa Alhamisi jioni haimaanishi kwamba Ufaransa inajiondoa katika ukanda wa Sahel lakini itapunguza vikosi vyake.

Emmanuel Macron alizungumzia "wanajeshi wa Ufaransa watapunguzwa kutoka zaidi ya 5,000 leo hadi mia kadhaa". Alitaja pia kufungwa kwa baadhi ya vituo vya jeshi la Ufaransa bila kubainisha vituo hivyo. Wazo ni kulenga tu vita dhidi ya ugaidi na sio tena kutoa ulinzi katika maeneo makubwa ambapo nchi husika zinajaribu kudhibiti hali ya mambo.

Na kufanya hivyo ndani ya muungano wa kimataifa. Ushirikiano uliowekwa karibu na kikosi cha Ulaya Takouba, kilichozinduliwa mwezi Machi 2020, na "kimetolewa wito wa kuimarisha vikosi vyake" alisema Emmanuel Macron. Ufaransa itabaki kuwa uti wa mgongo wa kikosi hiki ambacho majeshi mengine ya Afrika na ya kimataifa yatashirikishwa.