BURUNDI

Evariste Ndayishimiye: "Ni wakati wa kupitia vikwazo vya Ulaya dhidi ya Burundi"

Rais wa Burundi Evariste Ndayishimiye, wakati wa mahojiano yake na RFI na France 24.
Rais wa Burundi Evariste Ndayishimiye, wakati wa mahojiano yake na RFI na France 24. © RFI/France 24

Kwa mara ya kwanza tangu aingie madarakani, rais wa Burundi Evariste Ndayishimiye amekubali kufanya mahojiano marefu kwa vyombo vya habari vya kigeni. Kwa hili, ameamua kufanya mahojiano na RFI na France 24.

Matangazo ya kibiashara

Rais wa Burundi amehojiwa na mwanahabari wa RFI mjini Kinshasa, Sonia Rolley, na mwandishi wa France 24 huko Kinshasa, Clément Bonnerot. Amezungumzia hasa juu ya haki za binadamu nchini Burundi, kuanza tena kwa mazungumzo kati ay Burundi na Umoja wa Ulaya (EU) na hali ya uhusiano kati ya nchi yake na nchi jirani ya Rwanda.

Rais wa Burundi Evariste Ndayishimiye amekamilisha ziara ya siku mbili mjini Kinshasa, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, kwa mwaliko wa mwenzake wa DR Congo Félix Tshisekedi. Ilikuwa ziara nzuri kwa lengo kuboresha na kuimarisha ujirani mwema.

Ndayishimiye ataka ujirani mwema na majirani zake

Tofauti na mtangulizi wake, rais wa Burundi anajaribu kutazama jinsi ya kurejesha na kuboresha mahusiano na majirani zake na anataka kushirikian tena na washirika wake wa jadi, hata kama swala la vizuizi kwenye nafasi ya mfumo wa demokrasia linaendelea kuwa suala lenye mwiba. Wakati huo huo Maafisa kadhaa wa Burundi bado wako chini ya vikwazo vya  Umoja wa Ulaya.

Suala la vikwazo vilivyowekwa na Umoja wa Ulaya bado linaleta wasiwasi mkubwa. Rais Ndayishimiye ameliitaja mara kadhaa katika mahojiano na RFI na France 24. "Ni wakati wa kupitia uamuzi huu, sioni sababu za vikwazo hivi", amebaini rais wa Burundi, lakini amekumbusha kuwa mazungumzo tayari yameanza, ikiwa ni pamoja na maswala ya haki za binadamu. "Watatuambia wapi kuna kasoro, lakini sote mtazamo ni mmoja," aameongeza rais Ndayishimiye. "Sote tunataka kulindwa kwa haki za binadamu na utawala bora," amesema.

Ndayishimiye hakubaliani na kuwepo kwa visa vya watu kutoweka

Alipoulizwa juu ya kukamatwa kwa wapinzani na hasa wafuasi na makada wa chama cha Agathon Rwasa, rais Ndayishimyie amebaini kwamba "wahalifu wanataka kujificha katika vyama vya siasa". Na kuongeza: "Mhalifu ni mhalifu tu, hana chama cha siasa".

Kwa upande mwingine, amekanusha kuwepo kwa visa vya watu kutoweka. "Ninachojua ni kwamba kuna wahalifu wanaojificha nchini Rwanda na watu wanasema wametoweka," amesema Evariste Ndayishimiye, huku akihakikisha kwamba kuna "maendeleo mazuri" katika uhusiano wake na nchi jirani ya Rwanda, akizungumzia hatua za mwisho zilizochukuliwa hivi karibuni na pande zote mbili.