Sudan Kusini - Usalama

Jeshi Sudan Kusini lasema hali ya usalama imeimarika

Msemaji wa jeshi nchini Sudan Kusini, Meja jenerali Lul Ruai Koang
Msemaji wa jeshi nchini Sudan Kusini, Meja jenerali Lul Ruai Koang © Benson Wakoli

Kundi la waasi la National Salvation Front (NAS) linaloongozwa na Thomas Cirilo, bado ni tishio kwa usalama wa taifa  nchini Sudan Kusini, hasa katika eneo la Great Equatoria, haya ni kwa mjibu wa    msemaji wa jeshi hilo Meja Lul Ruai Koang.

Matangazo ya kibiashara

Meja jenerali Koang katika mahajiano na RFI Kiswahili, amesema kundi la NAS limekuwa likitekeleza mashambulizi kwa misingi ya kisiasa, na kutatiza usalama eneo zima la Equatoria, kama vile eneo la kati na magaharibi.

Meja jenerali Koang hata hivyo anasema hali ya usalama nchini Sudan Kusini haiwezi kulinganishwa na awali kabla ya kutiwa saini kwa mkataba wa amani, akisema mkataba huo umechangia kuimarika kwa hali ya usalama nchini Sudan Kusini. 

Suluhu la utovu wa usalama

Kwa mjibu wa Meja jenerali  Koang serikali inatumia mbinu zote kushawishi makundi ya waasi kusitisha vita, ikiwemo kushawishi makundi hayo kujiunga na serikali ili kuafikia suluhu la kisiasa ambalo limekuwa donda dugu nchini Sudan Kusini.

 Koang anasema hata hivyo vikosi vya serikali vinalazimika kuyakabili makundi ya waasi pale ambapo yanaokena kutekeleza misimamo yao mikali, ila serikali haijafanikiwa kufanya hivyo katika sehemu zote za nchi zinazokumbwa na utovu wa usalama.

Katika maeneo ya Yei na Equatoria meja jenerali Koang, anasema viongozi wa dini wanatumika kuhakikisha hali ya amani inashuhudiwa maeneo hayo.

Mkataba wa amani  wa Juba

 Kuhusiana na tuhuma za baadhi ya raia kuwa mkataba wa amani kati ya rais Salva Kiiri na hasimu wake wa kisiasa Riek Machar, unasalia katika jiji kuu la Juba pekee, Meja jenerali Koang anakanusha madai hayo akiwataka raia kutambua nini chanzo cha utovu wa usalama maeneo yao.

Kaong anasema baadhi ya maeneo yamekuwa yakishuhudia utovu wa usalama kutokana na swala la wizi wa mifugo na anasema hilo limetokea hata katika mataifa jiarani kama vile Kenya, huku akiwataka raia kukumbatia mkataba wa amani ili kumaliza uhasama wa kijamii.

Kaong hata hivyo anasema serikali inalenga kuwapokonya raia silaha pindi baada ya mkataba wa amani kutekelezwa vikalifu ili kumaliza swala la raia kuwashambulia wenzao na kuiba mifugo.

Kufunzu kwa kurutu wa Jeshi

Meja jenerali Koang, anasema karibuni kurutu wa jeshi wa upande wa serikali na waasi ambao wamekuwa katika  kambi kwa muda mrefu watafuzu chini ya kipindi cha mwezi moja ujao, na serikali inalenga kutumia wanajeshi hao katika kusuluhisha swala na utovu wa usalama nchini humo, idadi ya kurutu hao ikikadiriwa kuwa takirbani wanajeshi 53,000.

Tatizo kuu kwa kurutu hao kufuzu limekuwa sare na silaha, Koang akisema sare zimepatikana changamoto ikisalia silaha kutokana na Sudan kusini kuwekewa vikwazo vya silaha na jamii ya kimataifa, baada ya taifa hilo kutumbukia kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe mwaka 2013.

Kuhusu swala la Sudan Kusini Kuwekewa vikwazo, Meja jenerali Kaong, anakiri kuwa limelemaza pakubwa operesheni za jeshi kwani hata wanajeshi hawana silaha za kisasa kukabili adui.

Wanajeshi wengine wakipokea mafunzo bila kuwa na silaha, na wengine wana silaha zilizovunjika, Kaong akisema hilo limekuwa changamoto kwao.

Koang anasema juhudi za Sudan Kusini kutaka vikwazo dhidi yake kuondolewa hazijafua dafu, kwani serikali imepewa masharti mengi kutimiza kabla ya kuondolewa vikwazo hivyo.

Baadhi ya masharti hayo ni pamoja na kuwajibisha maafisa wa usalama wanaotuhumiwa  kuhusika katika ukiukaji wa haki za kibadamu na kuruhusu mashirika ya umoja wa mataifa kutoa huduma kwa raia nchini humo bila msharti mengi.

Kaong hata hivyo anasema kuna mwanga mbeleni kwani tayari serikali imetambuliwa katika juhudi zake za kusitisha usajili wa watoto katika jeshi la taifa hilo.

Mgawanyiko ndani ya Jeshi

Meja jenerali Koang amekanusha taarifa za kuwepo mgawanyiko ndani ya jeshi, akisema hali ambayo imekuwepo ni baadhi ya makamanda kuasi jeshi la serikali na kujiunga na makundi ya waasi kila mara wanapopatikana na makosa na hatua kuchukuliwa dhidi yao.

Koang akitolea mfano wa jenerali Stephen Borel ol yang’ ambaye aliondoka katika jeshi la Serikali na kujiunga na waasi wa kundi la South Sudan United Front.

Hata hivyo Koang amekiri kuwepo kwa ugumu wa kuunganisha jeshi la serikali na lile la waasi, akisema hawajui wanajeshi wa upande wa waasi watajiunga na serikali wakiwa na malengo yapi.

vifo vya madereva wa masafa marefu

 Meje jenerali Koang amewahakikishia madereva wa masafa marefu usalama wao, hasa baada ya baadhi yao kuuawa na watu wenye silaha, akisema kila hatua zimechukuliwa kuzuia visa vya madereva kuuawa.

Koang kadhalika amesema serikali imetambua sehemu ambazo wanajeshi wa serikali wamekuwa wakiweka vizuizi barabarani na kuchukua rushwa kutoka kwa madereva wa masafa marefu akisema hayo yote yameshughulikiwa, na kwamba baadhi ya wahusika tayari wamechukuliwa hatua za kinidhamu.