SAHEL-USALAMA

Jeshi la Ufaransa latangaza vifo vya maafisa 2 wa kundi la kigaidi la EIGS Sahel

Makao makuu ya jeshi la Ufaransa latangaza vifo vya maafisa wakuu wawili wa EIGS.
Makao makuu ya jeshi la Ufaransa latangaza vifo vya maafisa wakuu wawili wa EIGS. © AFP/File

Makao makuu ya jeshi la Ufaransa limetangaza Alhamisi jioni wiki hii vifo vya maafisa wawili wakuu wa kundi la kigaidi la EIGS. Maafisa wawili wakuu wa shirika la kigaidi la Islamic State katika Grand Sahara walipigwa risasi usiku wa Jumatano kuamkia Alhamisi, na vikosi vya Operesheni Barkhane, kaskazini mashariki mwa Mali.

Matangazo ya kibiashara

Kulingana na makao makuu ya jeshi la Ufaransa, wawili hao walipigwa risasi kusini mwa mji wa Ménaka. Mmoja anaitwa Rhissa al-Sahraoui, aliyetajwa kama mshirika wa karibu na waminifu wa kiongozi wa kundi la Islamic State katika Grand Sahara. Anasemekana kuwa na jukumu muhimu katika kuajiri na kutoa mafunzo kwa wapiganaji wenye silaha. Na inasemekana pia alishiriki katika shambulio la Inatès dhidi ya vikosi vya Niger mwezi wa Desemba 2019, ambalo lilisababisha vifo vya wanajeshi zaidi ya 80 wa Niger. Wakati huo serikali ilitangaza siku tatu za maombolezo ya kitaifa.

Kada mwingine wa kundi la EIGS ambaye jeshi la Ufaransa limesema lilimpiga risasi ni Abou Abderrahmane al-Sahraoui. Kulingana na makao makuu ya jeshi la Ufaransa, alikuwa na jukumu la mamlaka ya maadili kwani alikuwa akitunga sheria na kutoa hukumu kali kama hukumu ya kifo.

Wakati wa operesheni ya majeshi ya Ufaransa ambayo iliwaangamiza, nyaraka muhimu ziliripotiwa kukamatwa. Jeshi la Ufaransa linasema operesheni kama hiyo itaendelea kuwasaka wanajihadi.