MALI-SIASA

Mali: Mtu aliyejaribu kumuua rais wa mpito afariki dunia akiwa kizuizini

Rais wa mpito wa Mali Assimi Goïta (akivamlia nguo yenye rangi ya samawati) katika Msikiti Mkuu wa Bamako, muda mfupi kabla ya kulengwa na jaribio la mauaji, Julai 20.
Rais wa mpito wa Mali Assimi Goïta (akivamlia nguo yenye rangi ya samawati) katika Msikiti Mkuu wa Bamako, muda mfupi kabla ya kulengwa na jaribio la mauaji, Julai 20. Malick KONATE AFP

Mtu anayetuhumiwa kujaribu kumuua raisa wa mpito wa Mali Kanali Assimi Goïta, katika Msikiti Mkuu wa Bamako Jumanne ya wiki hii iliyopita, alifariki dunia akiwa chini ya ulinzi wa polisi Jumapili Julai 25, serikali ya Mali imetangaza katika taarifa.

Matangazo ya kibiashara

Yote yalianza saa sita mchana Jumapili Julai 25. Chanzo cha usalama nchini Mali kiliwaambia waandishi wa habari kuwa afya ya mshambuliaji wa rais wa mpito imedhoofika. Yuko hospitalini. Mchana, Waziri Mkuu wa Mali Choguel Maïga alikutana na rais wa mpito, Kanali Assimi Goïta. Wengi wanajiuliza iwapo wawili hao walijadili mada hii.

Muda mfupi baadaye, kifo cha mshambuliaji wa Kanali Goïta kilitangazwa. Sababu ya kifo chake ni ipi? Taarifa rasmi haielezi kuhusiana na kifo chake, lakini inasema kumeagizwa maiti ifanyiwe uchunguzi kupitia vipimo vya damu kubaini sababu ya kifo chake.

Uchunguzi unaendelea

Kwa upande wa serikali wanasema, kifo hiki hakizuii kuendelea kwa uchunguzi, hasa "kwani ushuhuda wa kwanza uliokusanywa unaonyesha kuwa mtu huyo alishirikiana na wengine kwa kujaribu kumuua rais wa mpito". Mamlaka nchini Mali inaamini kwamba kuna watu wengine wanaohusika katika jaribio la kumuua mkuu wa nchi.

Lakini kwa kukosekana kwa mshukiwa mkuu, ambaye alifariki dunia, baadhi wanaweza kujaribiwa kutilia shaka taarifa ya serikali. Ili kuweka mambo sawa, serikali na mahakama vinapaswa kuweka mambo wazi.