DRC-SIASA

DRC : Mvutano waendelea kujitokeza kuhusu uteuzi wa mwenyekiti wa CENI

Mwanamke akipita karibu na makao makuu ya Tume Huru ya Kitaifa ya Uchaguzi (CENI) Novemba 5, 2017 huko Kinshasa.
Mwanamke akipita karibu na makao makuu ya Tume Huru ya Kitaifa ya Uchaguzi (CENI) Novemba 5, 2017 huko Kinshasa. JOHN WESSELS / AFP

Viongozi wa kidini wameendelea kuvutana nchini Jamhuri ya kidemkorasia ya Congo kuhusu uteuzi wa mkuu wa tume huru ya uchaguzi CENI ambapo kuanzia mapema leo asubuhi wanatakiwa kukutana kuendelea na mazungumzo ili kupatikana kwa muafaka.

Matangazo ya kibiashara

Mwenyekiti wa Baraza la maaskofu wa kanisa Katoliki, Askofu Marcel Utembi, amewatolea wito viongozi wa kiroho kuwasili mapema hii leo katika eneo la mkutano kwa kuanza tena mazungumzo yenye lengo la kupatikana kwa muafaka juu ya uteuzi wa mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi, CENI.

Vikao vya shughuli hiyo vilisitishwa tangu Julai 27 baada ya viongozi wa madhehebu ya dini kushindwa kukubaliana juu ya uteuzi wa mwenyekiti wa Tume Huru ya Kitaifa ya Uchaguzi (CENI).

Kanisa Katoliki lilikuwa limeamba kupewa muda zaidi.

Madhehebu sita ya kidini (Kanisa la Orthodox nchini DR Congo, Kanisa la Yesu Kristo hapa duniani kupitia mjumbe wake maalum Simon Kimbangu (EJCSK), Jumuiya ya Kiislamu nchini DRC (COMICO), Kanisa la Uamsho wa Kongo (ERC), Muungano wa Makanisa Huru ya Kongo (UEIC) na Jeshi la Wokovu) baadaye walikutana katika makao makuu ya Tume ya Uadilifu na Usuluhishi wa Uchaguzi (CIME).

Madhehebu haya ya kidini yalitangaza Julai 27 jioni kwamba walikuwa wamemteua mgombea wa jukwaa lao kuwa mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi (CENI). Uteuzi huo ulifanywa kwa kukosekana kwa Kanisa Katoliki na Kanisa la Kristo nchini Kongo (ECC), ambao walisema kwamba kikao cha Jumanne kilisitishwa na kwamba kazi inapaswa kuanza tena Jumatano.

Kwa kuwa wameshindwa kufikia makubaliano juu ya mgombea mmoja, madhehebu ya kidini basi yalitafuta usuluhishi kutoka kwa spika wa Bunge la Kitaifa Christophe Mboso, ambae alikutana na pande mbili Kanisa Katoliki na lile la kiprotestanti pamoja na madhehebu sita na kuwataka kuendelea na mazungumzo ili kupatikana muafaka, na hivyo kuwapa muda wa saa 48 kumaliza tofauti zao na kutangaza jina la mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi.