ETHIOPIA-AFYA

UNICEF: Zaidi ya watoto 100,000 Tigray hatarini kupoteza maisha kwa utapiamlo

Kambi ya Emba Dansu, iliyopewa jina la shule ya msingi katika mji wa Shire ambako wakaazi wa eneo L Tigray Magharibi wamekimbilia, katika mkoa wa Tigray nchini Ethiopia, Mei 2021.
Kambi ya Emba Dansu, iliyopewa jina la shule ya msingi katika mji wa Shire ambako wakaazi wa eneo L Tigray Magharibi wamekimbilia, katika mkoa wa Tigray nchini Ethiopia, Mei 2021. © RFI/Sébastien Németh

Zaidi ya watoto 100,000 katika eneo la Tigray la Ethiopia, eneo la mapigano, wako katika hatari ya lishe inayohatarisha maisha katika miezi 12 ijayo, msemaji wa shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia watoto na wanawake katika mataifa yanayoendelea, UNICEF amesema Ijumaa wiki hii.

Matangazo ya kibiashara

Marixie Mercado, akirudi kutoka Tigray, amebaini kwamba mmoja kati ya wanawake wawili wajawazito au wanaonyonyesha wanakabiliwa na utapiamlo mkali, na kuwafanya wao na watoto wao kuathirika zaidi na magonjwa.

"Hofu yetu mbaya juu ya afya na ustawi wa watoto katika eneo hili lenye migogoro kaskazini mwa Ethiopia imethibitishwa," amesema katika mkutano wa Umoja wa Mataifa huko Geneva. Ameongeza kuwa hakukuwa na makadirio ya vifo na ametoa wito kwa nchi mbali mbali kutoa misaada ya kibinadamu bila kizuizi na misaada hiyo iweze kuwafikia walengwa.

Mapigano katika eneo hilo yalizuka kati ya serikali kuu ya Ethiopia na waasi wa Tigray People's Liberation Front (TPLF) mwezi Novemba mwezi liyopita. TPLF tangu wakati huo imedhibiti tena sehemu nyingi za jimbo hilo, lakini misaada mingi bado imezuiwa.

Msemaji wa Waziri Mkuu Abiy Ahmed, Billene Seyoum alisema katika mkutano na waandishi wa habari wiki hii kwamba vizuizi vyote vya misaada huko Tigray vilikuwa vikiangaliwa kwa karibu na serikali.

Wiki mbili zilizopita, msafara wa malori zaidi ya 200 kutoka Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa, WFP, uliweza kufika Mekelle, mji mkuu wa mkoa wa Tigray, lakini kulingana na Tomson Phiri, msemaji wa WFP, "ni kama tone la maji baharini" .

"Tunahitaji angalau malori 100 kusafiri hadi Tigray kila siku ikiwa tutapata nafasi ya kubadili hali mbaya ambayo tunayo leo," amesema.