CAR-USALAMA

Jamhuri ya Afrika ya Kati: Uhalifu mkubwa waripotiwa kaskazini magharibi mwa nchi

Kaskazini magharibi ni ngome ya kundi la waasi la 3R, linapigana na vikosi vya jeshi vya Jamhuri ya Afrika ya Kati.
Kaskazini magharibi ni ngome ya kundi la waasi la 3R, linapigana na vikosi vya jeshi vya Jamhuri ya Afrika ya Kati. AFP - CAMILLE LAFFONT

Hali ya usalama inazidi kuzorota kaskazini Magharibi mwa Jamhuri ya Afrika ya Kati, ngome kuu ya upinzani dhidi ya vikosi. Ripoti zinabaini kuepo kwa visa unyanyasaji mkubwa, makundi ya waasi kutoka Jamhuri ya Afrika ya Kati na wanajeshi wa Urusi wanaosaidia vikosi vya serikali wanahusishwa katika uhalifu huo. Karibu wahanga wote ni raia wa kawaida.

Matangazo ya kibiashara

Mauaji ya watu wengi, ubakaji, vijiji vilivyoteketezwa kwa moto, shambulio la helikopta, hivyo ni baadhi ya visa vinavyoripotiwa Kaskazini Magharibi mwa Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Vyanzo vya usalama vinathibitisha ongezeko la visa hivyo katika wiki za hivi karibuni, lakini ni vigumu kwa mashirika ya kutoa misaada kufika eneo hilo. Tume ya Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, MINUSCA, hivi karibuni ililazimika kusitisha shughuli zake za kuondoa mabomu katika eneo hilo.

Kanda hiyo, yenye madini mengi, ni ngome ya kundi la waasi la 3R, ambalo linapambana vikali na vikosi vya jeshi vya serikali. Siku ya Jumamosi, kundi hili lenye silaha, linaloshtumiwa kuhusika na uhalifu na ulipizaji kisasi dhidi ya raia, lilitoa taarifa likiwatuhumu wanamgambo wa Urusi ambao wanasaidia vikosi vya serikali kwa "mauaji" kadhaa, dhidi ya watu kutoka jamii za Fulani na Gbayan.

Waasi walitangaza zaidi ya raia 100 waliouawa. Idadi ambayo haijathibitishwa. "Habari za uzusi", kulingana na msemaji wa ofisi ya rais, Waziri Albert Yaloke Mokpeme, ambaye hata hivyo anathibitisha kukamatwa kwa wapiganaji kadhaa kutoka kundi la 3R upande wa mpaka wa Cameroon.