LIBYA-SIASA

Libya: Jumuiya ya kimataifa yatishia kuwachukulia vikwazo wale wanaozuia uchaguzi

Viongozi wa dunia wakihudhuria mkutano wa kimataifa kuhusu Libya
Viongozi wa dunia wakihudhuria mkutano wa kimataifa kuhusu Libya © Niger Presidency

Viongozi wa nchi zenye nguvu duniani wamekutana Ijumaa mjini Paris katika sehemu ya mkutano kuhusu Libya na kutishia kuwawekea vikwazo watu ambao, ndani au nje ya nchi hiyo, "wanajaribu kuzuia, kuweka mashakani au kuvuruga" uchaguzi uliopangwa kufanyika Desemba 24, kulingana na taarifa ya mkutano huo.

Matangazo ya kibiashara

Pia wametoa wito kwa uchaguzi wa rais na wabunge, uchaguzi wa kwanza katika historia ya nchi hii, kuwa wa "kawaida", "jumuishi" na "wa kuaminika", taarifa hiyo imebaini.

Umoja wa Mataifa unauchukulia uchaguzi huu kama fursa muhimu ya kumaliza machafuko ya Libya ambayo yamedumu kwa mwongo mmoja tangu mapinduzi ya mwaka 2011 yaliyoungwa mkono na muungano wa kujihami wa NATO.

Bado haiko wazi iwapo uchaguzi huo wa urais na bunge utafanyika huku zikiwa zimesalia wiki sita tu, kwa kuwa bado kuna mizozo kati ya pande zinazohasimiana mashariki na magharibi mwa Libya na mihimili ya kisiasa kuhusiana na sheria zinazosimamia ratiba ya uchaguzi na anayeweza kugombea.

Kwa wafadhili wa mkutano huu, kipaumbele ni kuepuka kuahirisha uchaguzi au kupinga matokeo ya uchaguzi. Kwa sababu kutoka Tripoli hadi Tobruk, mtafaruku umeanza kujitokeza wakati uchaguzi wa urais ukikaribia. Wale wana hofu ya kutengwa wanataka wasikike.

Mchakato wa maridhiano ulioanzishwa mwaka 2020 na jumuiya ya kimataifa umeanza kupoteza nguvu. Ili kuepuka kusababisha mzozo mpya kama ilivyokuwa baada ya uchaguzi wa 2014, jumuiya ya kimataifa inakusudia kutoa wito kwa Walibya kujitolea kupiga kura ya uwazi na ya umoja kadri inavyowezekana.