SUDAN-USALAMA

Sudan: Umoja wa Mataifa walaani vurugu "za aibu" dhidi ya waandamanaji

Waandamanaji wanaounga mkono demokrasia wakiweka vizuizi katika mitaa ya Khartoum. Novemba 17, 2021.
Waandamanaji wanaounga mkono demokrasia wakiweka vizuizi katika mitaa ya Khartoum. Novemba 17, 2021. © AFP

Vurugu za vikosi vya usalama vya Sudan dhidi ya waandamanaji wasio na silaha "ni aibu kabisa," ameshutumu Michelle Bachelet, Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Kibinadamu, baada ya mauaji ya Jumatano na ghasia zaidi kuendelea Alhamisi wiki hii.

Matangazo ya kibiashara

"Ni aibu sana kuona risasi za moto zinatumiwa dhidi ya waandamanaji jana (Jumatano) baada ya maombi yetu mengi kwa wanajeshi na vikosi vya usalama kutotumia nguvu kupita kiasi dhidi ya waandamanaji," amesema Bi. Bachelet katika taarifa yake.

Siku ya Jumatano Novemba 17, waandamanaji wasiopungua 15 walipigwa risasi na kufa wakati wa maandamano mjini Khartoum kupinga mapinduzi ya kijeshi ya Jenerali al-Burhan. 

Kulingana na vyanzo vya hospitali vinavyounga mkono demokrasia, vimebaini kwamba watu kadhaa wamejeruhiwa, lakii wengi wamejeruhiwa vibaya. Hata hivyo vyombo vya usalama vimekanusha madai kuwa vilifyatua risasi za moto.

Ripoti ya hivi punde imebaini kwamba Jumatano ilikuwa siku mbaya zaidi tangu mapinduzi ya Oktoba 25. Katika Hospitali ya Royal Care, jioni, angalau vifo 15 vilirekodiwa, huku ikiongeza kuwa wengi walipigwa risasi. Hospitali ya Royal Care ilikuwa ikijiandaa kuwapokea wagonjwa kutoka wilaya ya Bourri.

Mzozo wa umwagaji damu kati ya raia na wanajeshi unaendelea. Chama cha Wataalamu wa Sudan kinashutumu polisi kwa "mauaji ya kukusudia". Kulingana na chama cha madaktari, waathiriwa wengi walipigwa risasi, huku vikosi vya usalama vikilenga "kichwa, kifua au shingo". Chama hicho kinawatuhumu wanajeshi wa Jenerali Burhan kwa kuwakimbiza waandamanaji hadi hospitalini na kuwarushia mabomu ya machozi watu waliojeruhiwa na magari ya wagonjwa.