BURKINA FASO-USALAMA

Burkina Faso: Msafara wa wanajeshi wa Ufaransa wazuiwa kwenye lango la mji wa Kaya

Msafara wa magari ya wanajeshi wa Ufaransa katika eneo la vijijini kaskazini mwa Burkina Faso.
Msafara wa magari ya wanajeshi wa Ufaransa katika eneo la vijijini kaskazini mwa Burkina Faso. © MICHELE CATTANI / AFP

Tangu Alhamisi jioni, Novemba 18, vijana kutoka mji wa Kaya, katika eneo la Centre-Nord, wamekuwa wakiandamana kutaka kuondoka kwa wanajeshi wa Ufaransa nchini Burkina Faso.

Matangazo ya kibiashara

Vijana hao wanakataa kuruhusu msafara wa kijeshi wa Ufaransa kupita wakati unatakiwa kuingia nchini Niger. Magari haya tayari yalikuwa yamezuiwa katika miji ya Bobo na Ouagadougou. Na hali ya Kaya kwa sasa iko katika sintofahamu.

Kaya haikuwahi kushuhudia tukio hilo hapo awali. Barabara za mji huo kwa sasa zimefungwa. Kulingana na wakazi kadhaa, katika barabara kutoka Ouagadougou kuelekea Kaya, na kutoka Kaya kuelekea Dori, msongamano wa magari unachukua zaidi ya kilomita ishirini. Watu binafsi na magari ya kibiashara yamesimama kabisa.

Boukaré Ouédraogo, meya wa mji wa Kaya anakadiria kuwa leo waandamanaji wanaozuia msafara wa Ufaransa ni elfu kadhaa. Idadi ya vijana hao imeongezeka baada ya vijana kutoka miji jirani, pamoja na wanafunzi wa shule za Kaya kujiunga vijana wenzao. "Hakuna wanafunzi au waalimu wanaoripoti shleni," amebaini Boukaré Ouédraogo.

Alhamisi jioni na mapema Ijumaa hii asubuhi, gavana wa eneo la Centre-Nord na meya wa jiji la Kaya walijaribu kuanzisha upatanishi, lakini bila mafanikio. Vijana wa Kaya, ambao wamejikusanya kadri muda unavyokwenda, bado msimamo wao: wanajeshi wa Ufaransa lazima waondoke, masuala ya kuvuka mji huo, hamna.

Maandamano yanafanyika kwa amani. Kikosi cha walinzi wa jamhuri kimepiga kambi kwenye eneo la tukio. “Bado tunatakiwa kutafuta mwafaka, ili maisha yaendelee,” amesema mkazi wa Kaya.

Makao makuu ay jeshi la Ufaransa kufikia sasa hayajaongea chochote kuhusiana na tukio hilo.