SUDAN

Abdalla Hamdock arejeshewa Uwaziri Mkuu nchini Sudan

Utawala wa kijeshi nchini Sudan umemrejesha madarakani, Waziri Mkuu Abdalla Hamdock, baada ya mkataba wa makubaliano wa kisiasa kati ya jeshi na Hamdock kusainiwa.

Waziri Mkuu wa Sudan  Abdallah Hamdock  11 Desemba  2019 akiwa jijini Khartoum.
Waziri Mkuu wa Sudan Abdallah Hamdock 11 Desemba 2019 akiwa jijini Khartoum. ASHRAF SHAZLY / AFP
Matangazo ya kibiashara

Abdel Fattah al Burhan, kiongozi aliyeongoza mapinduzi nchini Sudan, amekubali kutia saini kurejesha utawala wa serikali ya mpito na kumrejesha Hamdock madarakani baada kuongoza mapinduzi mwezi mmoja uliopita.

Makubaliano hayo pia yanaruhusu kuachiwa huru kwa wafungwa wote wa kisiasa, waliokamatwa baada ya mapinduzi ya serikali, na pia mkataba wa mwaka 2019 kuendelea kutumika kufanikisha serikali ya mpito.

Waziri mkuu Abdalla Hamdock amesema kwa kusaini makubaliano hayo mapya analenga kumaliza maandamano ambayo yamekuwa yakishuhudiwa nchini humo.

Nilipokubali wadhifa huu kama kaimu waziri mkuu, nilijua hali itakuwa ngumu, hata hivyo kwa pamoja sote tutafika mahala salama, na tutazuia taifa letu kuelekea tusipopajua, tunafaa kuja pamoja na kuamua nani ataongoza Sudan.

Naye kiongozi wa jeshi Jenerali Abdel Fattah al Burhan  ametaja makubaliano hayo kama njia ya kweli ya kidemokrasia ya serikali ya mpito kurejesha uwatala wa kiraia.

Kupitia makubaliano haya ya kisiasa tunatoa mwelekeo kwa njia kamili ya mpito na ya kidemokrasia, kama wanavyotaka watu wetu, na kile tulitaka mwanzo wa april mwaka 2019, tunashukuru raia wote wa Sudan kwa kujitolea, tumejitolea kuungana na nikawaida kuwa na maoni tofauti, miongoni mwetu.

Haya yanajiri wakati vyama kadhaa ya kisiasa na baadhi ya mashirika ya kiraia nchini humo yakipinga makubaliano hayo ya kisiasa.