ETHIOPIA-USALAMA

Ethiopia: Abiy Ahmed abadili kauli baada ya waasi kusonga mbele

Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed katika uzinduzi wa muhula wake wa pili mjini Addis Ababa Oktoba 4, 2021.
Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed katika uzinduzi wa muhula wake wa pili mjini Addis Ababa Oktoba 4, 2021. AFP - AMANUEL SILESHI

Wakati muungano wa waasi kutoka Tigraya na Oromo wakiwa kilomita 200 na mji mkuu wa Ethiopia, Waziri Mkuu Abiy Ahmed ametangaza kwamba atakwenda kwenye uwanja wa vita yeye binafsi kuongoza ulinzi wa mji mkuu.

Matangazo ya kibiashara

Ilikuwa ni baada ya kikao cha kamati kuu ya chama chake, Prosperity Party, ambapo Waziri Mkuu Abiy Ahmed amefahamisha kwamba kuanzia Jumanne hii, Novemba 23, yeye binafsi "atakwenda kuongoza majeshi " katika uwanja wa vita dhidi ya waasi. "Wale wanaotaka kuwa miongoni mwa watoto wa Ethiopia waliosifiwa na historia, simameni leo kwa ajili ya nchi yenu," amesema.

Baada ya kutangaza hali ya hatari Novemba 2, Abiy Ahmed, mwanajeshi wa zamani, amechagua kutoa hotuba ya kitaifa, inayokumbusha viapo vya kulitumikia taifa wakati wa vita vya wafalme wa zamani wa Ethiopia. Kauli hii inakuja, wakati muungano wa waasi kutoka Oromo na Tigray walioapa kumuondoa wamesema wanasonga mbele kuelekea Addis Ababa na hasa tayari wameudhibiti mji wa Shewa Robit, kilomita 200 kutoka mji mkuu.

"Hatuwezi kuendelea hivi"

Kwa upande wake, Waziri wa Ulinzi wa Ethiopia, Abraham Belay, pia amebaini kwamba vikosi vya kijeshi hatimaye vitatumia "hatua tofauti", lakini bila maelezo zaidi. "Hatuwezi kuendelea hivi," amesema kwa urahisi.

Jeshi la Ethiopia likiwa limedhoofika sana, vita hivi sasa vinaendeshwa katika maeneo mbalimbali hasa na wanamgambo na vikosi vya majimbo. Na juhudi za kidiplomasia za Marekani na Umoja wa Afrika zinaonekana kukwama hivi leo.