SUDAN-SIASA

Sudan: Watu wengi waendelea kukamatwa licha ya makubaliano

Maandamano mjini Khartoum baada ya makubaliano ya Novemba 21.
Maandamano mjini Khartoum baada ya makubaliano ya Novemba 21. - AFP

Kwa mujibu wa masharti ya makubaliano kati ya Abdallah Hamdok na Jenerali Al-Burhane, wahusika wa kisiasa wameachiliwa huru kama vile Omar al-Digair, kiongozi wa chama cha Sudanese Congress Party au Yasir Arman wa chama cha Sudan People's Liberation Movement, Faisal Mohammed Saleh, waziri wa zamani wa habari, pamoja na Saddiq Saddiq al-Mahdi, wa chama cha Umma. Lakini wafungwa wengi wanasalia gerezani na kamata kamata inaendelea kulingana na mawakili.

Matangazo ya kibiashara

Min Hagak ni muungano wa wanasheria wanaharakati wanaojaribu kutoa usaidizi wa kisheria kwa wale wanaozuiliwa na mamlaka. Kwa mujibu wa Shaheen al-Sharif, makubaliano yaliyotiwa saini siku ya Jumapili hayatoi hakikisho.

" Ni wawakilishi sita tu wa vyama vya siasa ambao waliachiliwa. Lakini idadi kubwa kati ya wanasiasa na wafuasi wao pamoja na wanaharakati kadhaa bado wanazuiliwa. Baadhi wanakabiliwa na mashtaka makubwa. Kwa upande mwingine, hakuna mwanachama wa kamati za upinzani aliyekamatwa ambaye ameachiliwa huru licha ya makubaliano yaliyotiwa saini siku ya Jumapili. Siku hiyo, watu wengine walikamatwa. kamata kamata inaendelea. "

Kuanzia wanaharakati, maafisa, waandishi wa habari au watu wanaojaribu kuandamana wamekamatwa kote nchini,muungano huo wa wanasheria umebaini.

"Tangu Jumapili, kumekuwa na kamata kamata kwa wanachama wa kamati za upinzani huko Gedaref, Kassala, el-Obeid na huko Wad Madani. Mara nyingi, wanaonekana katika mahakama za dharura, kama ilivyokuwa wakati wa Omar al-Bashir. Wengine wanadaiwa kuhatarisha usalama, wengine wanakabiliwa na mashtaka mazito zaidi kama vile kulitusi jeshi au idara ya ujasusi na kuishia jela moja kwa moja. "

Kulingana na hesabu ya mawakili hawa, kumekuwepo na watu wasiopungua 300 waliokamatwa katika mji mkuu wa Khartoum tangu mapinduzi na karibu elfu moja kote nchini.