Tetemeko la ardhi New Zealand: watalii waondolewa kwa helikopta
Jumanne hii Novemba 15 helikopta za jeshi zimeanza kuwandoa zaidi ya watalii elfu moja waliokwama kutokana na tetemeko kubwa la ardhi linaloendelea kuiathiri nchi ya New Zealand.
Imechapishwa:
Kundi la kwanza la watalii 1,200 waliokwama katika mji wa bahari wa Kaikoura katika Kisiwa cha Kusini, wameanza kusafirishwa kwa ndege na vyombo vingine vya jeshi.
Chombo cha majini, HMNZS Canterbury, chenye uwezo wa kusafirisha mamia ya watu, pia kinatarajiwa kuwasili katika eneo hilo, Jumatano wiki hii.
Mji wa Kaikoura umeendelea kukumbwa na tetemeko la ardhi lenye ukubwa wa 7.8 katika kiwango cha Richter ambalo lilipiga New Zealand na kusababisha vifo vya watu wawili Jumatatu wiki hii.
Mji wa Kaikoura hauingiliki kutokana na maporomoko makubwa ya udongo ambayo yameharibu barabara na reli.
Kwa mujibu wa polisi, hifadhi ya maji imeanza kushuka huku mamia ya watu wakiendelea kuishi katika vituo vilivyotengwa kwa ajili ya shughuli ya uokoaji.
Watu wapatao 2,000 wanaishi katika mji wa Kaikoura.