DRC-EBOLA-AFYA

Kampeni ya kutoa chanjo ya kudhibiti maambukizi ya Ebola kuanza DRC

Timu ya madaktari nayopambana na Ebola katika Hospitali ya Bikoro nchini DRC.
Timu ya madaktari nayopambana na Ebola katika Hospitali ya Bikoro nchini DRC. REUTERS/Jean Robert N'Kengo

Wafanyakazi wa afya nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Jumatatu wiki hii wanaanza kampeni rasmi ya kutoa chanjo ya kudhibiti maambukizi ya virusi hatari vya ugonjwa wa Ebola, wakati huu shirika la Afya duniani WHO likisema maambukizi ya DRC sio hatari kidunia kwa sasa.

Matangazo ya kibiashara

Mwishoni mwa juma jumla ya dozi elfu 4 zilisafirishwa hadi kwenye mji wa Mbandaka ambako juma lililopita mtu mmoja aliripotiwa kuwa na maambukizi ikiwa ni kesi ya kwanza kugunduliwa kwenye maeneo ya mjini na tangu kuthibitishwa kuibuka kwa ugonjwa huo.

Waziri wa afya nchini DRC Oly Ilunga amethibitisha kuwasili kwa chanjo hizo na kuongeza kuwa kuna uwezekano mkubwa wa kuripotiwa maambukizi zaidi kwenye maeneo mengine lakini akisisitiza kuwa ugonjwa huo umedhibitiwa kwa sasa.

Jumla ya dozi laki 3 za chanjo za ugonjwa huo zimeahidiwa kutolewa na nchi washirika wa DRC huku Shirika la Afya Duniani (WHO) likisema linafikiria pia kutumia chanjo iliyotengenezwa na kampuni nyingine ya Johnson and Johnson.

Mpaka sasa jumla ya watu 25 wamethibitishwa kupoteza maisha kaskazini magharibi mwa nchi ya DRC kwenye mji wa Bikoro huku watu zaidi ya 45 wakiripotiwa kuwa na maambukizi ya virusi vya ugonjwa huu.

Kumekuwa na hofu kuwa ugonjwa huu huenda ukafika kwenye jiji la Kinshasa kupitia mto Congo ambao unatenganisha jiji hilo na mji wa Mbandaka.