AFRIKA-MAZINGIRA

Nchi nyingi Afrika zakabiliwa na visa vya ukataji miti

Nchini nyingi barani Afrika zinakabiliwa na hatari ya kugeuka jangwa ikiwa ukataji miti kiholela, uchomaji makaa na uzoaji changarawe mitoni utaendelea bila kudhibitiwa.

Msitu wa Mau nchini Kenya.
Msitu wa Mau nchini Kenya. © AFP/Roberto SCHMIDT
Matangazo ya kibiashara

Wataalamu wa mazingira wanaonya kwamba kasi ambayo watu wanakata miti inaangamiza misitu, kukausha vyanzo vya maji na kuathiri hali ya hewa.

Hofu ya wanamazingira ni kuwa ukataji miti unaendelea bila miti mipya kupandwa jambo ambalo ni hatari kwa mazingira katika nchi ambazo idadi ya watu inaendelea kuongezeka.

Kulingana na shirika la Umoja wa Mataifa, kila nchi inapaswa kuhakikisha ina asilimia 10 ya misitu jambo ambalo wataalamu wa mazingira wanasema ni ndoto barani Afrika, hasa nchi za Afrika ya Kati na Mashariki.

Misitu mikubwa kote imevamiwa na wafanyabiashara wanaokata miti kiholela kupasua mbao, kuchoma makaa na kupata mashamba bila kujali athari za vitendo vyao kwa mazingira.