DRC-WHO-EBOLA-AFYA

DRC: Mgonjwa wa kwanza wa Ebola Goma afariki dunia

Mtu ambaye amekuwa ameambukizwa virusi vya Ebola jiji Goma, katika Mkoa wa Kivu Kaskazini, mashariki mwa DRC, amefariki dunia alipokuwa akisafirishwa kwenda katika mji wa Butembo, chanzo rasmi kimesema leo Jumanne.

Maafisa wa afya wa kituo cha matibabu ya Ebola cha Butembo, Machi 9, 2019, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Maafisa wa afya wa kituo cha matibabu ya Ebola cha Butembo, Machi 9, 2019, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. © AFP
Matangazo ya kibiashara

"Kwa masikitiko makubwa ninaweza kuthibitisha kifo cha mgonjwa aliyeambukizwa virusi vya Ebola wakati alipokuwa akisafirishwa kwenda Butembo," ambako kunapatikana kituo cha kukabiliana na ugonjwa huo, Gavana wa mkoa wa Kivu Kaskazini Carly Nzanzu amewaambia waandishi wa habari.

Kwa mujibu wa wizara ya afya ya DRC, mtu huyo ambaye ni Mchungaji alisafiri umbali wa kilomita zaidi ya 200 kutoka Butembo hadi Goma kwa basi, na inasadikiwa kuwa alikuwa amekutana na watu wenye ugonjwa Ebola.

Goma ni mji wenye watu milioni moja, pamoja na muingiliano wa watu kutoka miji mingine ya nchi hiyo na nchi jirani ya Rwanda. Kamati ya dharura ya shirika la Afya Duniani (WHO) inatarajiwa kukutana tena katika siku zijazo kuamua kama Ebola imekuwa tishio la kimataifa.

Kuuawa kwa watu wawili miongoni mwa maafisa wanaopambana dhidi ya ugonjwa wa Ebola katika mkowa wa Kivu Kaskazini na kupatikana kwa mtu mwenye virusi vya Ebola katika mji wa Goma, kumezua sintofahamu kwenye ajenda ya mkutano wa shirika la Afya Duniani uliofanyika Jumatatu, Julai 15, kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa. Ikiwa ugonjwa huo umefika Goma, unaweza pia kufika katika mji mkuu Kinshasa.

Waziri wa Afya wa DRC, Oly Ilunga amewahakikishia wananchi wake. Amebaini kwamba hakuna hatari ya kusambaa kwa ugonjwa wa Ebola kwa kiwango kikubwa tangu kuonekana kwa virusi vya ugonjwa huo.

Ebola huwaathiri binaadamu kupitia mgusano na wanyama walioathirika kama tumbili, na popo wa msituni.

Watu huambukizwa kwa njia ya kugusana, njia ya mdomo na pua, pia kwa njia ya damu, matapishi, kinyesi, majimaji ya kwenye mwili wa mtu mwenye Ebola.

Ebola ni ugonjwa unaoambukizwa na virusi ambapo aliyepata maambukizi hupata dalili za homa, uchovu, maumivu ya viungo na koo.