DRC-EBOLA-AFYA

Kesi mpya 14 za maambukizi ya virusi vya Ebola zatangazwa DRC

Maafisa wa afya wa kituo cha matibabu ya Ebola cha Butembo, Machi 9, 2019, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Maafisa wa afya wa kituo cha matibabu ya Ebola cha Butembo, Machi 9, 2019, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. © AFP

Wizara ya afya nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, imetangaza maambukizi mapya 14 ya Ebola katika mkoa wa Kivu Kaskazini na Ituri. Maambukizi hayo mapya, yameripotiwa kutokea katika mji wa Beni, Mandima na Mutwanga.

Matangazo ya kibiashara

Mbali na maambukizi hayo, watu wengine sita waliokuwa wameabukizwa virusi vya Ebola wamefariki dunia.

Ugonjwa wa Ebola umesababisha vifo vya watu zaidi ya 1,700 na wengine zaidi ya 2000 kuambikizwa tangu mwezi Agosti mwaka 2018.

Hivi karibuni shirika la Afya Duniani (WHO) lilitangaza "dharura ya kiafya" duniani kwa sababu ya ugonjwa wa Ebola nchini DRC ambao umeua watu 1,700 tangu mwezi Agosti mwaka jana.

Tahadhari hii ilitolewa baada ya mtu wa kwanza kufariki dunia baada ya kuambukizwa virusi vya Ebola katika mji wa Goma, mji unaotembelewa na watu kutoka nchi mbalimbali za Maziwa Makuu.

Shirika la Afya Duniani linasema virusi vya ugonjwa huo vinaendelea kusambaa kutoka Afrika Magharibi na sasa kufikia nchi nyingine. Mataifa mengi yameimarisha ukaguzi katika viwanja vya ndege.

Lakini shirika hilo limesema hatari ya ugonjwa huo kusambaa nje ya Congo si kubwa.

Mlipuko wa Ebola ni ugonjwa wa pili kwa ukubwa katika historia ya nchi hiyo, ulianza mwezi Agosti na inaathiri mikoa miwili nchini DRC, Kivu Kaskazini na Ituri.

Zaidi ya watu 2500 wameathiriwa na ugonjwa huo na theluthi mbili kati yao wamepoteza maisha.

Ilichukua siku 224 kwa idadi ya walioathirika kufika 1,000 , lakini ndani ya siku 71 zaidi idadi ilifika 2,000.

Watu takribani 12 huripotiwa kupata ugonjwa huo kila siku.