DRC-EBOLA-AFYA

Ugonjwa wa Ebola wandelea kusabaisha vifo mashariki mwa DRC

DRC: Mtoto apewa chanzo dhidi ya Ebola katika kituo cha afya cha Himbi, Goma, 17 Julai 2019.
DRC: Mtoto apewa chanzo dhidi ya Ebola katika kituo cha afya cha Himbi, Goma, 17 Julai 2019. REUTERS/Olivia Acland

Mtoto mmoja amefariki kutokana na ugonjwa wa Ebola mashariki mwa nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kwenye jimbo la Kivu Kusini, akiwa ni mtu wa pili kufa kwenye jimbo hilo tangu ugonjwa huo uanze kuenea mashariki mwa nchi.

Matangazo ya kibiashara

Tangazo la wiki iliyopita la uwepo wa wagonjwa kwenye jimbo la Kivu Kusini, limezidisha wasiwasi kuwa huenda virusi vya ugonjwa huu hatari vikaenea hata kwenye nchi jirani zinazopakana na DRC.

Tangazo la hapo jana limesema mtoto wa miaka 7 amefariki mwishoni mwa juma lililopita kwenye mji wa Mwenga, kifo chake kikiwa ni cha pili kuthibitishwa baada ya awali mwanamke mmoja kufariki akiwa ametokea kwenye mji wa Beni jimboni Kivu Kaskazini.

Msemaji wa serikali katika mkoa wa Kivu Kusini Claude Bahizire, amesema mtoto wa miezi saba wa mama aliyefariki anaendelea kupatiwa matibabu huku akitoa wito kwa watu waliikutana na mama huyo kujisalimisha katika vituo maalumu vya Ebola.

Wanawake wengine wawili waliokutana na mwanamke aliyefariki nao wanaendelea kupatiwa matibabu ya ugonjwa wa Ebola ambao mpaka sasa umegharimu maisha ya watu elfu 1 na 900.