Coronavirus: Berlin, London na Paris wapendekeza kusaidia Iran
Imechapishwa:
Ujerumani, Ufaransa na Uingereza wametoa mapendekezo kwa Iran kuitolea msaada wa Euro milioni 5 pamoja na msaada wa vifaa kusaidia kupambana na kuenea kwa virusi vya ugonjwa hatari unaofahamika kama Covid-19, vyanzo rasmi kutoka nchi hizo tatu vimetangaza.
Nchi hizi tatu za Ulaya ambazo pia zilitia saini kwenye mkataba wa mpango wa nyuklia wa Iran, zitatoa msaada wao kupitia Shirika la Afya Duniani (WHO) na mashirika mengine ya Umoja wa Mataifa, vyanz hivyo vimeendelea.
"Tunatoa pendekezo kwa Iran kuisaidia kifedha na kuipa vifaa ili kupambana na kuenea haraka kwa virusi vya ugonjwa wa Covid-19. Vifaa hivyo vitasafirishwa kwa dharura kwa ndege Machi 2 na ni pamoja na vifaa vya kufanya vipimo na vinginevyo, ikiwa ni pamoja na maski za kujikinga na maambukizi ya virusi hivyo, "zimesema nchi hizo tatu.
"Nchi zetu tatu pia tumeamua kutoa, kupitia shirika la WHO na mashirika mengine ya Umoja wa Mataifa, misaada ya ziada ya karibu Euro milioni 5 kusaidia kupambana na janga la Covid-19 lililoathiri Iran."
Iran imekuwa moja ya chanzo kikuu cha kuenea kwa ugonjwa huo ambao ulizuka nchini China mwishoni mwa Desemba, na vifo vipya 66 vimeripotiwa nchini humo pamoja na kesi zaidi ya 1,500 za maambukizi.