Mgonjwa aliyepona Ebola aruhusiwa kwenda nyumbani Beni
Mtu wa mwisho aliyepona ugonjwa wa virusi vya Ebola huko Beni, katika Mkoa wa Kivu Kaskazini, Mashariki mwa DRC, ameruhusiwa Jumanne wiki hii kuondoka kituo cha matibabu cha Ebola (CTE) na kujiunga na familia yake.
Imechapishwa:
Mratibu wa kituo kinachopambana na ugonjwa wa virusi vya Ebola huko Beni mjini, Daktari John Kombe amesema ana furaha kubwa na huo ni ushindi walioupata, hasa kwa kituo cha matibabu cha Ebola (CTE) Beni.
"Nina furaha kubwa kwa sababu imekuwa safari ndefu lakini hatumaanishi kuwa ugonjwa huu umekwisha. Kwa sababu hapo awali tulikuwa na maeneo 29 ya afya, eneo pekee ambalo lilikuwa na wagonjwa walioambukizwa virusi hivyo ni eneo la afya la Beni. Lakini tumefurahi kwa kazi ya pamoja; ni kazi ambayo ilijumuisha jamii, wataalamu ambao walikuja kusaidia na wale ambao tulikuta hapa Beni, viongozi tawala, viongozi wa kisiasa, kwa hivyo ni kazi iliyomuhusu kila mmoja na haya ndio matunda ya kazi hii, "Daktari John Kombe amesema.
Hata hivyo, amewataka wananchi kuwa makini na kuheshimu sheria za usafi hadi itakapotangazwa kwamba mripuko wa ugonjwa huo umemalizika.
"Tutaendelea kuwasiliana, nadhani wazo ni kwamba tunaweza kuwa makini na tunaweza kushikamana pamoja ili tusipotezi chochote. Ujumbe ambao tunapenda kutuma kwa jamii yetu yote huko Beni ni kusema kwamba tumeshinda, kushinda Ebola kwanza ni kukubali na kuelewa kuwa Ebola ipo; tukubali kupelekwa katika vituo maalum ili tuweze kuhudumiwa vilivyo. "