ISRAELI-PALESTINA-CORONA-AFYA

Coronavirus: Watalii wapigwa marufuku kuingia Betlehemu

Watalii wanasubiri uamuzi wa Israeli baada ya kuzuiliwa kuingia Betlehemu katika Ukingo wa Magharibi unaoshikiliwa na polisi ya Israeli Machi 6, 2020.
Watalii wanasubiri uamuzi wa Israeli baada ya kuzuiliwa kuingia Betlehemu katika Ukingo wa Magharibi unaoshikiliwa na polisi ya Israeli Machi 6, 2020. © AFP

Mamlaka nchini Israeli imezuia watalii kuingia Betlehemu, mji mkuu wa watalii katika maeneo ya Palestina kutokana na kugunduliwa kwa kesi za maambukizi ya virusi vya ugonjwa wa Covid-19.

Matangazo ya kibiashara

Hali hiyo imepelekea viongozi wa eneo hilo kutangaza hali ya dharura ya kiafya katika ukanda huo.

Kulingana na mwandishi wa habari wa AFP, karibu mabasi ishirini ya watalii yamezuiwa kwenye kituo cha ukaguzi mahali pa kuingilia katika mji wa Bethlehemu, mji unaopatikana kilomita kumi na Jerusalem.

"Ninathibitisha kwamba mabasi ya watalii hayawezi kuingia Betlehemu," Mick Rosenfeld, msemaji wa polisi ya Israeli ameliambia shirika la Habari la AFP.

"Kufuatia kugunduliwa kwa kesi ya maambukizi huko Bethlehemu, uamuzi ulichukuliwa jana na Wizara ya Ulinzi ya Israeli kwa kushirikiana na Mamlaka ya Palestina kuzuia safari za nenda rudi kuelekea au kutoka katika mji huu", ameongeza afisa huyo.

Watu saba wamepatikana na virusi vya Covid-19 katika Ukingo wa Magharibi, kwa mujibu wa maafisa wa Palestina ambao Alhamisi walitangaza hali ya dharura ya siku 30.